• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Beki wa Gor Mahia hatimaye afanyiwa upasuaji

Beki wa Gor Mahia hatimaye afanyiwa upasuaji

NA CECIL ODONGO

MLINZI wa Gor Mahia Philemon Otieno hatimaye alifanyiwa upasuaji wa goti Alhamisi wiki jana kutokana na jeraha alilopata akichezea timu ya taifa, Harambee Stars miezi miwili iliyopita.

Otieno alieleza Taifa Leo kwamba alifanyiwa upasuaji huo katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuchangisha Sh450,000 zilizohitajika kutoka kwa familia, mashabiki, wachezaji na fedha ambazo amekuwa akidunduliza.

Mwanadimba huyo aliumia wakati wa mechi ya kufuzu kwa kipute cha taifa Bingwa Afrika 2020 (CHAN) kinachoshirikisha wachezaji wa klabu za nyumbani pekee mwezi Agosti.

“Ndio nilifanyiwa upasuaji Alhamisi wiki jana na nimekuwa nikiyafuata maagizo ya daktari kwa kufanya mazoezi mepesi kila siku. Nashukuru familia, marafiki, mashabiki kwa kunichangia na kunisaidia kufikisha kiwango cha fedha kilichohitajika. Ahsanteni sana kwa walioniombea ikizingatiwa ulikuwa wakati mgumu mno na nilihisi uchungu sana,” akasema Otieno.

Mwanasoka huyo maarufu miongoni mwa mashabiki kama ‘Mbish’ alifichua kwamba hakupokea msaada wowote wa kifedha kutoka kwa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) na klabu yake ya Gor Mahia.

Aidha alishukuru Muungano wa Kupigania Maslahi ya Wanasoka Nchini (KFWA) kwa kumsaidia pamoja na wanasoka wenzake kambini mwa K’Ogalo.

“Kando na KFWA, nina shukran za kipekee kwa wachezaji Musa Mohamed, Michael Olunga, Joash Onyango, Johana Omollo na Aboud Omar. Kwa kweli wao ni marafiki wa dhati pamoja na wengine wote waliojinyima na kunitumia fedha zao,” akaongeza.

Beki huyo hata hivyo, alisisitiza kwamba hana kisasi au machungu na afisa yeyote wa FKF na kufichua kwamba bado yupo tayari kushirikishwa kwenye timu ya Harambee Stars siku zijazo licha ya kutelekezwa na shirikisho hilo.

“Sina kinyongo na mtu yeyote na mimi pamoja na familia yangu tumeamua kuzika suala hili kwenye kaburi la sahau,” akasema.

You can share this post!

Mizozo kuhusu mipaka yaendelea kusababisha mauti

TULIZIDIWA: Spurs yala kipigo kikali Uefa

adminleo