Beki wa zamani wa Man-United apokezwa mikoba ya ukocha kambini mwa Atlanta United
Na MASHIRIKA
KIKOSI cha Atlanta kinachoshiriki soka ya Major League Soccer (MLS) nchini Amerika kimemteua beki wa zamani wa Manchester United, Gabriel Heinze kuwa kocha wao kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.
Sogora huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 42 aliwahi pia kuchezea Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa na miamba wa soka ya Uhispania, Real Madrid.
Heinze aliwahi kudhibiti mikoba ya kikosi cha Velez Sarsfield kwa kipindi cha misimu miwili kabla ya kuagana nacho mwishoni mwa msimu wa 2019-20.
“Hii ni historia kubwa katika kikosi cha Atlanta United. Gabriel ni mojawapo ya makocha wa haiba kubwa zaidi katika soka ya Amerika Kusini. Ni tija na fahari tele kwamba aliteua kujiunga nasi,” akasema Rais wa Atlanta, Darren Eales.
Hadi kuteuliwa kwa Gabriel, kiungo wa zamani wa Aberdeen, Stephen Glass ndiye alikuwa kocha mshikilizi wa kikosi cha Atlanta baada ya kuondoka kwa Frank de Boer mnamo Julai 2020.
“Nafurahi kuikubali fursa hii ya kunoa kikosi cha Atlanta United. Naamini kwamba falsafa yangu ya ukufunzi inawiana na ya klabu hii,” akaongeza.