Michezo

Berlin Marathon: Mkenya Kotut aibuka wa pili Muethiopia Mengesha akitamba

Na GEOFFREY ANENE September 29th, 2024 1 min read

WAKENYA wamekosa lao kwenye mbio za Berlin Marathon baada ya Waethiopia Milkesa Mengesha na Tigist Ketema kunyakua mataji nchini Ujerumani mnamo Jumapili, Septemba 29, 2024.

Mengesha alikata utepe kwa saa 2:03:17 baada ya kumtoka mpinzani wake wa karibu Cybrian Kotut kutoka Kenya katika kilomita ya mwisho.

Kotut aliridhika na nafasi ya pili kwa 2:03:22 na kufuatiwa na Muethiopia Haymanot Alew (2:03:31), Mkenya Stephen Kiprop (2:03:37) na Muethiopia Hailemariyam Kiros (2:04:35), mtawalia.

Mkenya mwingine ndani ya 10-bora ni Enock Onchari katika nafasi ya tisa kwa 2:05:53.

Watimkaji wakongwe Eliud Kipchoge na Kenenisa Bekele walikuwa wametawala Berlin Marathon tangu mwaka 2015, lakini hawakushiriki makala haya ya 50 baada ya kukimbia kwenye Michezo ya Olimpiki mjini Paris nchini Ufaransa mwezi uliopita. Bingwa mara tano Kipchoge alikuwa bingwa mtetezi.

Mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia mbio za 21km, Kibiwott Kandie aliyekuwa amepigiwa upatu kutwaa taji, alikuwa katika kundi la kwanza kwa kipindi kirefu kabla ya kupoteza vita katika kilomita saba za mwisho na kumaliza nambari 12 kwa 2:06:46.

Wakenya pia hawakuwa na lao katika kitengo cha wanawake baada ya Tigist Ketema kuibuka na ushindi kwa 2:16:42 akifuatiwa na Waethiopia wenzake Mestawot Fikir (2:18:48) na Bosena Mulatie (2:19:00).