• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Binti kocha wa karate anavyonoa vipaji

Binti kocha wa karate anavyonoa vipaji

Na LAWRENCE ONGARO

UNAPOFIKA katika shule ya msingi ya Kenyatta, Makongeni, Thika, kaunti ya Kiambu, utapata vijana chipukizi wa kati ya miaka mitano na 12 wakifanya mazoezi ya Karate katika Klabu ya Young Dragons.

Kocha wa kike anayenoa chipukizi hao ni Elizabeth Rukwaro, ambaye amejitolea kuona ya kwamba anakuza vipaji vya vijana hao wachanga.

Mwanakarate huyo aliye na ukanda wa 2nd Dan, mkanda mweusi anasema kuwa lengo lake kuu ni kuona ya kwamba amedumisha nidhamu miongoni mwa vijana hawa.

“Baada ya kuona wengi wa vijana hao wakibarizi mitaani bila kufanya lolote, nilionelea nianzishe klabu ya karate ya vijana chipukizi. Lengo kuu ni kuona vijana hawa wanapata ujuzi wa kujikinga kutokana na uvamizi wa adui,” alikariri Rukwaro.

Anasema ilipofika mwaka wa 2010 alilazimika kutembelea wazazi wa vijana hao ili wampatie ruhusa kirasmi ili kuchukua jukumu la kuwapa mazoezi ya karate.

Hivi majuzi vijana hao chipukizi walisafiri hadi uingereza ambapo walishiriki katika pambano la (Funakoshi World karate Championship 2019) ambapo kikosi cha Kenya kilifanya maajabu.

Katika fainali ya mashindano hayo chipukizi hao wa Kenya walizoa jumla ya medali 20 katika viwango tofauti na kupokea vikombe vinne.

“Ama kwa hakika tunarudisha shukrani zetu kwa mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliyefadhili safari nzima ya kikosi hicho kupitia wakfu wa (Jungle Foundation).

“Wazazi wa chipukizi hao wamepongeza ufadhili huo wakisema ni hatua nzuri ya kuendeleza mchezo wa karate,” akasema Rukwaro.

Kocha huyo anafurahia juhudi zake akieleza kuwa mchezo huu umesaidia kuimarisha nidhamu miongoni mwa vijana wake shuleni na hata mitaani ambapo hata walimu wao katika shule ya msingi ya Kenyatta wanakosomea wameridhishwa na tabia za wanakarate hao.

“Kila mara baada ya kuwafanyisha mazoezi huwa ninawapa ushauri kwa dakika 30 kuhusu kujitenga na mambo maovu, dawa za kulevya na maswala ya kuwa na tabia njema,” aeleza mkufunzi huyo.

Kocha huyo amekuwa katika ulingo wa karate kwa zaidi ya miaka 20 na ni mmoja wa waamuzi wenye ujuzi zaidi katika mchezo huo hapa nchini.

Baadhi ya nchi amezuru akicheza mchezo huo ni Ghana, Rwanda, Uingereza, Afrika Kusini, India na Benin.

Anasema wakati mwingi yeye hufanya mazoezi mazito baada ya kutoka kazini jioni mwendo wa saa 11.

Anawahimiza wasichana kujitokeza kwa wingi kujifunza mchezo huo wa karate akisema una manufaa mengi ya kiafya, kitabia, na pia katika kuweka msingi bora wa siku za usoni.

You can share this post!

WANDERI: Rais binafsi ajipe jukumu la kuzima ufisadi

Kibera Blacks Stars yagonga City Stars

adminleo