Birgen na Kiplangat kutimka kwa fainali Birmingham, Uingereza
Na GEOFFREY ANENE
WAWAKILISHI wa Kenya katika mbio za mita 3,000 kwenye Riadha za Dunia za Ukumbini, Bethwell Birgen na Davis Kiplangat, wameingia fainali mjini Birmingham, Uingereza, Ijumaa.
Watatimka katika fainali Jumapili saa kumi na mbili jioni na dakika 35.
Kiplangat alimaliza mchujo wa pili katika nafasi ya pili nyuma ya Muethiopia Selemon Barega naye Birgen akafuzu kutoka mchujo wa kwanza kutokana na kasi yake nzuri baada ya michujo hiyo miwili kukimbiwa licha ya kumaliza kundi lake katika nafasi ya tano.
Barega alishinda mchujo wa pili kwa dakika 7:48.14. Alifuzu pamoja na Kiplangat (7:48.26), Mwitaliano Yassin Bouih (7:50.65) na Julian Oakley (New Zealand, 7:55.92) katika mchujo huo uliokuwa na wakimbiaji 11.
Mzawa wa Kenya, Paul Chelimo, ambaye ni raia wa Marekani, aliondolewa mashindanoni kwa uvunjaji sharia.
Birgen (7:45.06) alimaliza nyuma ya Waethiopia Yomif Kejelcha (bingwa mtetezi, 7:42.83) na Hagos Gebrhiwet (7:43.55), Mhispania Adel Mechaal (7:43.83) na Mbahraini Birhanu Balew (7:44.03). Mmoroko Youness Essalhi (7:45.07), Mjerumani Clemens Bleistein (7:49.01) na mzawa wa Kenya Shadrack Kipchirchir (Marekani, 7:57.08) pia walifuzu kutokana na muda wao.
Chelimo alikuwa mmoja wa wakimbiaji wakali waliotarajiwa kunyakua taji.