Michezo

Blatter na Platini kurejea mahakamani Uswisi kwa kesi ya ufisadi

Na MASHIRIKA, BENSON MATHEKA March 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Aliyekuwa rais wa FIFA, Sepp Blatter, na nyota wa soka wa Ufaransa, Michel Platini, watafika mahakamani Uswisi Jumanne kusikiliza uamuzi wa kesi iliyokomesha taaluma zao. Mahakama ya Rufaa  ya Mahakama ya Jinai ya Uswisi itapitia tena hukumu yao ya mwaka 2022 baada ya waendesha mashtaka wa shirikisho kupinga uamuzi wa kuwaachilia huru.

Kesi hiyo inahusu malipo ya mamilioni ya pesa aliyoyaidhinisha Blatter kwa Platini mwaka 2011. Wawili hao wanadai kuwa fedha hizo zilikuwa ada ya ushauri kwa kazi ambayo Platini alifanya kati ya 1998 na 2002, lakini malipo yake yalicheleweshwa kutokana na changamoto za kifedha za FIFA wakati huo.

Sakata hili ilifichuka mwaka 2015, Platini alipokuwa rais wa UEFA, na ilizima matumaini yake ya kumrithi Blatter kama kiongozi wa FIFA. Wote wawili walipigwa marufuku kujihusisha na soka kwa ukiukaji wa maadili.

Shtaka la mwaka 2022 lilidai kuwa Blatter na Platini walidanganya FIFA kuhusu malipo hayo, wakitumia uongo kwamba FIFA ilikuwa inadaiwa na Platini au alikuwa na haki ya kulipwa pesa hizo. Hata hivyo, mahakama ya awali iliamua kuwa maelezo yao ya “makubaliano ya maelewano” yalikuwa ya kuaminika, ikitia shaka madai ya mashtaka kuhusu udanganyifu.

Aliyekuwa rais wa FIFA, Sepp Blatter. PICHA|HISANI

Blatter, ambaye aliongoza FIFA kwa miaka 17 hadi 2015, amesisitiza kuwa hana hatia, akijitaja kuwa mhanga wa mateso ya kisiasa. Sasa akiwa na umri wa miaka 89 na afya dhaifu, anashikilia msimamo wake kuwa hakufanya kosa lolote. Platini, mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Ulaya mara tatu, pia anakanusha makosa yoyote, akisema fedha hizo zilikuwa ni malipo yaliyolimbikiza.

“Hakuna ufisadi, hakuna udanganyifu—hakuna kosa lolote,” alisema Platini mwanzoni mwa kesi ya rufaa. Wakili wake, Dominic Nellen, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kisiasa ili kumzuia Platini kuwa rais wa FIFA.

“Platini ndiye aliyekuwa na nafasi kubwa zaidi ya kumrithi Blatter, lakini mtu fulani alitaka kumzuia,” alisema Nellen.

Uamuzi wa mahakama utaamua ikiwa Blatter na Platini wataendelea kusafishwa majina yao au watapatikana na hatia, jambo ambalo linaweza kudhoofisha zaidi heshima zao.