Michezo

Blue Nile FC yaishinda maarifa Rhino FC

February 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO
KLABU ya Blue Nile FC iliikomoa Rhino FC kwa mabao 3-2 katika mechi safi ya Aberdare Regional League iliyoandaliwa uwanja wa Kibichoi Kiambu.
Licha ya  vijana wa Rhino kuchezea  Uwanja wa  nyumbani tena wanaouelewa vyema bado walishindwa kutamba mbele ya wageni hao.
Chipukizi wa Blue Nile ya kocha Salim Swaleh walijitupa dimbani kwa kishindo huku wakiihangaisha difensi ya wenyeji bila  shida.
Timu ya Blue Nile FC kabla ya kucheza mechi mojawapo ya Aberdare Regional League. Picha/ Lawrence Ongaro
Ilikuwa ni patashika ya hapa na pale na katika dakika ya 24 mvamizi matata wa Blue Nile, John Shiunwa alizititiga nyavu kwa kishindo.
Hata hivyo, Rhino ilifanya kweli na kurekebisha ngome yake ili vijana hao waweze kukabiliana vilivyo na wapinzani wao.
Kunako dakika ya 37 kiungo wa kutegemewa wa Rhino Peter Kimani alifanya kweli na kuipatia timu yake bao la kwanza.

Bao la pili  lilifumwa kimiani na mshambulizi matata Francis Kimani katika dakika ya 42.

Gongagonga

Kipindi cha lala salama vijana wa Blue Nile waligeuza msimamo wao wa ushambulizi huku wakizingatia  gongagonga za chini chini ambapo straika wao Joseph Mburu alionyesha umahiri wake wa kusakata  boli na kufunga  mabao mawili  mfululizo dakika ya  64 na 70.

Kocha wa Blue Nile anakiri ya kwamba vijana wake walipiga  soka safi iliyowapa matumaini ya kusonga mbele kwenye jedwali  la Ligi hiyo.

“Kwa sasa ninaongoza kwa alama tisa baada ya kuchapa mechi tano. Hata hivyo mechi ya hapo awali dhidi ya Ruiru Sports Academy tulilala mabao 2-0,” alisema kocha huyo.

Katika mechi nyingine ya Aberdare Regional League kwenye Kundi C timu ya BTL ya Ruiru iliichabanga Gataiyu FC kwa mabao 2-1 katika mechi iliyopigiwa uwanjani Ruiru.
Straika matata John Kimani wa BTL alifanya kweli na kufunga mabao yote mawili katika kipindi cha kwanza.
David Kimani alifunga bao la pekee la Gataiyu katika dakika ya 64.

Kwingineko, Mutomo FC ya Gatundu ililazimika kutoka sare ya 1-1 dhidi ya JYSA FC; nayo Maragua HomeBoyz ilitoka sare ya mabao 3-3 na Ruiru Sports Academy. Mechi hiyo ilipigiwa katika uwanja wa Ruiru.