Boateng abanduka Fiorentina
Na MASHIRIKA
KIUNGO wa zamani wa Barcelona na AC Milan, Kevin-Prince Boateng ameagana rasmi na Fiorentina na kujiunga na kikosi cha Monza kinachoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Italia (Serie B).
Nyota huyo mwenye umri wa 33 atakuwa huru kurefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa Monza kwa mwaka mmoja zaidi baada ya mkataba wa sasa kutamatika Juni 2021.
Boateng ambaye ni mzawa wa Ujerumani na raia wa Ghana, alivalia jezi za Besiktas ya Uturuki kwa nusu ya kampeni zote za msimu uliopita wa 2019-20.
Kwa kuingia katika sajili rasmi ya Monza, Boateng ambaye pia amewahi kucheza Tottenham Hotspur, Portsmounth na Schalke, anaungana sasa na mmiliki wa zamani wa AC Milan, Silvio Berlusconi.
Akiwa AC Milan, Boateng aliwaongoza AC Milan kutwaa taji la Serie A huku Berlusconi Adriano Galliani ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Monza wakiwa vinara wakuu wa Milan.
Kevin-Prince ni kakaye mkubwa beki matata wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Jerome Boateng.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO