Bodi ya uchaguzi wa FKF yatoa orodha ya mwisho ya wapigakura katika uchaguzi ujao
Na CHRIS ADUNGO
BODI ya Uchaguzi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) imetoa orodha ya mwisho ya klabu ambazo zitapiga kura katika uchaguzi wa kaunti na ule wa kitaifa.
Maafisa wapya kutoka kaunti 45 watachaguliwa na klabu ambazo zimekuwa zikishiriki mapambano mbalimbali ya soka ya humu nchini kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Nairobi, Kiambu, Kilifi, Mombasa, Kisumu, Migori na Nakuru zitakuwa na idadi kubwa ya wapiga kura hasa ikizingatiwa kwamba zina zaidi ya vikosi 30 kwa pamoja vitakavyopiga kura katika kiwango cha kaunti.
Uchaguzi unatarajiwa kuwa wa haraka katika Kaunti ya Murang’a iliyo na klabu tatu pekee huku Nyeri, Nyandarua, Taita-Taveta na Kirinyaga zikiwa na vikosi vitano kila moja.
Wajumbe 18 wa klabu za Ligi Kuu ya Kandanda humu nchini (FKFPL), 10 wa Ligi ya Kitaifa ya Supa (Betika NSL), 10 wa Ligi ya Daraja la Kwanza, watatu wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake (KWPL) na mmoja wa Ligi ya Wanawake daraja la kwanza; ndio watakaopiga kura katika uchaguzi wa kitaifa.
Chini ya Mwenyekiti Kentice Tikolo, bodi hiyo inatarajiwa Jumatano ya Agosti 26, 2020 kuchapisha orodha ya majina ya wajumbe halali ambao watapiga kura katika uchaguzi wa kaunti utakaofanyika Septemba 19, 2020. Uchaguzi wa kitaifa utaandaliwa Oktoba 17, 2020.
Wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali katika kiwango cha kaunti wana hadi Agosti 26 kuwasilisha stakabadhi zao kwa bodi ya uchaguzi wa FKF.