Bondia anayeinukia Lamu afichua ‘bullying’ ilimzindua kujijenga
NA KALUME KAZUNGU
MARA nyingi mtu hujipata akifanya vyema kwenye mchezo fulani, iwe ni kandanda, raga, netiboli, magongo, voliboli, tenisi, na masumbwi kutokana na mapenzi aliyo nayo kwenye mchezo husika.
Wengine hujipata hodari na kutia bidii kwenye nyanja fulani, hasa punde anapogundua kuwa fani hiyo ni talanta yake ya kuzaliwa.
Ila kuna wengine ambao hujipata wakiwika kwenye tasnia baada ya kusukumwa kufanya hivyo kutokana na yaliyompata maishani au wazazi kumshinikiza kufanya hivyo.
Katika kaunti ya Lamu, bondia anayeinukia, Ahmed Hamid,22, ni miongoni mwa waja ambao walijiingiza kwenye mchezo wa masumbwi baada ya kupitia madhila kutoka kwa wanafunzi wenzake wa shule moja ya upili eneo hilo.
Kulingana na Ahmed, madhila hayo, almaarufu ‘bullying’ yalimwacha na makovu nafsini mwake tangu alipojiunga na shule hiyo ya upili mnamo mwaka 2019 hadi kuhitimu kwake masomo ya sekondari mnamo 2022.
Ahmed kwa sasa ni miongoni mwa mabondia chipkizi karibu kumi ambao wanawika si haba kwenye klabu ya masumbwi ya Lamu Youth Boxing Club.
Wanamasumbwi hao hufanya mazoezi yao kwenye mtaa wa Mkomani, kisiwani Lamu.
Wako chini ya kocha Abdalla Feiswal, ambaye pia ni bondia mashuhuri aliyetamba na kuwakilisha Lamu kwenye kaunti zingine na hata nje ya nchi.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo Alhamisi, Ahmed alifichua kuwa wanafunzi wakubwa ambao walikuwa wamempiku kimadarasa walikuwa wakimkejeli na hata kumpigapiga kiholela punde alipojiunga na kidato cha kwanza kwenye shule husika.
Anasema wanafunzi hao wa vidato vya juu pia walipata mwanya mzuri wa kumdhulumu kutokana na udogo wake alionao kimwili.
“Nilipitia kichapo au bullying mbaya sana wakati nikiwa sekondari. Wanafunzi wakubwa wangu kiumri, kimadarasa na hata kiukubwa wa mwili walinitesa. Walinipiga ilhali wengine wakanilazimisha niwe nikiwasafishia malazi yao. Sikuwa na budi ila kufanya hayo kwa kuogopa kipigo cha mbwa,” akaeleza Ahmed.
Anasema mateso yaliendelea hadi alipoingia Kidato cha Pili ndipo yakapungua.
“Kutokana na hilo, nikaamua kamwe sitajihusisha na dhuluma kwa wanafunzi wadogo au wageni shuleni ila nitawakinga dhidi ya dhuluma zozote zile. Nilianza kufanya mazoezi ya mwili, ikiwemo kuinua vyuma ilmradi niujenge mwili wangu vyema. Kisha nilijiunga na klabu ya masumbwi shuleni, dhamira kuu ikiwa ni kupata ujuzi wa kujikinga mwenyewe binafsi na pia kuwatetea wanaodhulumiwa na kuwakinga,” akasema.
Baada ya kukamilisha kidato cha nne mnamo 2022, Ahmed alifululiza moja kwa moja kujiunga na timu ya masumbwi ya Lamu Youth Boxing Club ambayo inawika ndani na nje ya kisiwa cha Lamu.
Anasema ni bullying ambayo hadi sasa imefanya kutia fora mchezoni na kujijenga vilivyo.
“Kwa sasa nimewakilisha klabu yangu kwenye mashindano ya ndani kwa ndani, kushindwa na kushinda baadhi ya mechi, hivyo kuiletea timu yangu sifa kochokocho. Pia natarajia kwamba siku za usoni nitaweza kwenda kuzichapa nje ya Lamu n ahata katika ngazi za kitaifa na kimataifa,” akasema Ahmed.
Kocha Abdalla Feiswal alimtaja Ahmed kuwa kijana mwenye bidii na nidhamu mchezoni.
Bw Feiswal anasema endapo kijana huyo hatarudi nyuma atafikia upeo kwenye tasnia hiyo ya masumbwi.
“Mimi niko na wachezaji wa kutegemea kama watano hivi kwenye klabu yangu ninayofunza. Miongoni mwa hawa jina Ahmed Hamid halikosekani. Lakini wale mibabe kabisa ni wawili ambao ni Ali Omar na Abdulkadir Mohamed. Hivi tunavyoongea tayari tuko kaunti ya Kajiado tukiwakilisha Lamu kwenye mchezo wa ndondi,” akasema Bw Feiswal.
Baadhi ya changamoto ambazo kocha huyo anazitaja ni ukosefu wa ufadhili ili kuimarisha mchezo na wachezaji wake.
“Sisi hatuna eneo maalum la kufanyia mazoezi ya mchezo wetu wa ndondi. Tuko tu kwenye kiwanja nje ya nyumba yetu ambapo tumezingira kamba kuendeleza mazoezi. Miundomsingi ya masumbwi iko duni. Tungeomba wafadhili wajitokeze tusaidiwe ili tuufikishe mchezo wa ndoni wa Lamu mbali, iwe ni ngazi za kitaifa na kimataifa,” akasema Bw Feiswal.
Bondia Ali Omar alisema furaa yake ni kuona wahisani wakijitokeza Lamu, Kenya na kimataifa ili kuwadhamini na kuunawirisha mchezo wa masumbwi.
“Tuko na moyo wa kuuendeleza mchezo hadi kufikia kiwango cha juu kabisa. Ndondi imewapa vijana wengi shughuli na majukumu si haba, hivyo kuwakosesha muda wa kupoteza kwenda mitaani na vichochoroni kutumia dawa za kulevya. Hata kuna wengine tunaoshiriki nao mchezoni ambao waliweza kukombolewa kutoka kwa mihadarati na uhalifu mwingine kupitia ndondi. Ni mchezo wa maana na wa nidhamu,” akasema Bw Omar.