• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Borussia Dortmund wamfuta kazi kocha Favre baada ya kudhalilishwa na Stuttgart ligini

Borussia Dortmund wamfuta kazi kocha Favre baada ya kudhalilishwa na Stuttgart ligini

Na MASHIRIKA

BORUSSIA Dortmund wamemfuta kazi kocha Lucien Favre baada ya kikosi hicho kupokezwa kichapo cha 5-1 kutoka kwa Stuttgart katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) iliyowakutanisha mnamo Disemba 12, 2020 uwanjani Signal Iduna Park.

Kichapo hicho ambacho kilikuwa cha tatu kwa Dortmund kupokezwa katika jumla ya mechi tano za Bundesliga, kiliwaacha miamba hao wa soka ya Ujerumani katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 19, tano nyuma ya viongozi Bayern Munich.

Hata hivyo, Favre, 63, amewaongoza Dortmund kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kumaliza kampeni za Kundi E katika nafasi ya kwanza kwa alama 13, tatu zaidi kuliko nambari mbili Lazio ya Italia.

Favre ambaye ni raia wa Uswisi, amekuwa akidhibiti mikoba ya Dortmund tangu aagane na Nice ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Julai 2018.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na usimamizi wa Dortmund mnamo Disemba 13, 2020, Edin Terzic aliyekuwa msaidizi wa Favre ameteuliwa kuwa kocha mshikilizi hadi mwishoni mwa kampeni za msimu huu wa 2020-21.

“Hayo yalikuwa masaibu. Kichapo hicho kilituzamisha. Matokeo dhidi ya Stuttgart hayakuridhisha kabisa. Kikosi kilizembea katika kila idara. Hayo hayastahili kabisa kufanyika,” akasema Favre mwishoni mwa mchuano huo.

Chini ya Favre, Dortmund waliambulia nafasi ya pili mwishoni mwa kampeni za Bundesliga mnamo 2019-20.

You can share this post!

Wataka kilio cha wauguzi kisikilizwe kabla BBI

Kenya Cup haitakuwa mchezo msimu ujao – Chenge