Borussia Dortmund yasubiri Bayern au Real Madrid
Na MWANGI MUIRURI
KLABU ya Borussia Dortmund mnamo Jumanne iliibandua nje Paris Saint Germain (PSG) katika hatua ya nusu-faijali ya Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) kwa kuikung’uta bao 1-0.
Bao la Mats Hummels katika dakika ya 50 ndilo lilizika PSG katika kaburi la sahau la Uefa kwa msimu huu, ikitumwa kujaribu bahati katika msimu ujao.
Timu hizo mbili zilikutana katika uga wa Parc des Princes kwa awamu ya pili ya mtanange huo huku Dortmund ikiwa guu mbele kwa bao moja kwa nunge na baada ya kuongeza hilo la Jumanne usiku, mambo yakawa ni 2-0.
Ajabu ni kwamba, PSG ilipiga mashuti 30 katika mechi hiyo, matano yakilenga michuma lakini yakikosa uwezo wa kuzalisha bao hata moja.
Hata hivyo Dortmund huenda ikiwa na wasema kweli, watakiri kwamba iliponea, kwa kuwa mashuti manne yalipiga miamba ya goli na ulikuwa usiku wa mkosi ambapo mpira ulikataa tu kutikisa nyavu licha ya kutumwa kufanya hivyo kwa kila aina ya mbinu.
Dortmund ilipiga mashuti saba na ambapo matatu yalilenga michuma, moja likigeuka kuwa bao muhimu la ushindi.
PSG ilikuwa na umiliki wa mpira guuni kwa asilimia 70 huku Dortmund ikiwa na 30 pekee, pasi za PSG zikitandazwa kwa hesabu ya 659 nao Dortmund wakiwa na pasi za uhakika 295.
Sasa Dortmund itangoje udhia wa Jumatano usiku kati ya Bayern Munich na Real Madrid ambapo katika awamu ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 hivyo basi kuweka kipute hicho chao kuwa wazi kwa yeyote.
Iwapo timu ya Bayern itailemea Real Madrid, ina maana kwamba fainali itakuwa kati ya timu mbili za Ujerumani ambazo kwa sasa zinashiriki ligi kuu ya Bundesliga.
Hii ni hali ambayo inawafanya mashabiki wengi nje ya Ujerumani na marafiki wake kuonekana wakishabikia timu ya Real Madrid katika mechi yao ya ugani Santiago Bernabeu ili kulipa dimba hilo la Uefa upana wa usawa Ulaya katika uwaniaji wa taji hilo.