Michezo

Brigid Kosgei auma nje Delhi Half Marathon

November 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

BRIGID Kosgei ameambulia pakavu kwenye mbio za Airtel Delhi Half Marathon nchini India, Jumapili.

Mkenya huyo, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za marathon, alikuwa katika orodha ya watimkaji waliopigiwa upatu kutesa jijini Delhi, lakini hakuwa na lake akisalimu amri kabla ya kuzikamilisha.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka India, malkia huyo wa London Marathon hakumaliza mbio hizo za kilomita 21 baada ya kusumbuliwa na jeraha la mguu. “Alijiondoa baada ya kilomita ya nane kwa sababu hakuweza kuendelea kukimbia akiwa na uchungu mguuni,” ripoti hizo zilisema.

Kosgei alishangaza ulimwengu alipovunja rekodi ya dunia ya Muingereza Paula Radcliffe ya mbio za kilomita 42 iliyokuwa imedumu kwa miaka 17 alipokata utepe kwenye mbio za Chicago Marathon kwa saa 2:14:04 mwaka 2019. Nambari mbili Muethiopia Ababel Yeshaneh alimaliza kwa zaidi ya dakika sita (2:20:51) mjini Chicago.

Hapo Jumapili, mbio za Delhi zilipata washindi wapya kupitia kwa Waethiopia Amdework Walelegn na Yalemzerf Yehualaw walioshinda kitengo cha wanaume na kile cha wanawake kwa rekodi ya Delhi Half ya dakika 58:53 na saa 1:04:46, mtawalia. Walizawadiwa Sh2.9 milioni kila mmoja tuzo ya washindi. Waliongezwa Sh1.1 milioni kila mmoja kwa kuvunja rekodi za Delhi Half zilizoshikiliwa na Waethiopia Guye Adola (59:06) na Tsehay Gemechu (1:06:00).

Bingwa wa dunia wa mbio za kilomita 42 Ruth Chepng’etich kutoka Kenya alikamilisha sekunde 20 nyuma ya Yehualaw (1:05:06) naye Leonard Barsoton akawa Mkenya wa kwanza katika kitengo cha wanaume katika nafasi ya tano kwa dakika 59:10.

Wakenya hawajashinda Delhi Half tangu Eliud Kipchoge na Cynthia Limo wabebe mataji ya mwaka 2016 na 2015, mtawalia.

Matokeo (10-bora):

Wanaume

Amdework Walelegn (Ethiopia) dakika 58:53

Andamlak Belihu (Ethiopia) 58:54

Stephen Kissa (Uganda) 58:56

Muktar Edris (Ethiopia) 59:04

Leonard Barsoton (Kenya) 59:10

Tesfahun Akalnew (Ethiopia) 59:22

Victor Kiplangat (Uganda) 59:26

Shadrack Kimining (Kenya) 59:51

Abrar Osman (Eritrea) saa 1:00:10

Avinash Sable (India) 1:00:30

Wanawake

Yalemzerf Yehualaw (Ethiopia) saa 1:04:46

Ruth Chepngetich (Kenya) 1:05:06

Ababel Yeshaneh (Ethiopia) 1:06:43

Irene Cheptai (Kenya) 1:06:43

Tsehay Gemechu (Ethiopia) 1:07:16

Eva Cherono (Kenya) 1:07:18

Nazret Weldu (Eritrea) 1:09:47

Mimi Belete (Bahrain) 1:09:50

Bekelech Gudeta (Ethiopia) 1:09:54

Brillian Kipkoech (Kenya) 1:11:39

Mgao wa tuzo:

1. Sh2.9 milioni, 2. Sh2.2 milioni, 3. Sh1.4 milioni, 4. Sh880, 392, 5.Sh660,294, 6. Sh550,245, 7.Sh440,196, 8. Sh330,147, 9.Sh220,098, 10.Sh110,049.