Michezo

Bruno Fernandes afunga na kupoteza penalti

June 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

VIUNGO Bruno Fernandes na Paul Pogba waliwajibishwa na Manchester United kwa mara ya kwanza katika mchuano mmoja katika mechi mbili za kirafiki zilizowakutanisha na West Bromwich Albion.

Mnamo Juni 12, West Brom walisafiri ugani Old Trafford ambako walishiriki mechi za kirafiki zilizodumu kwa jumla ya dakika 120 kadri vikosi hivyo vinavyojiandaa kwa marejeo ya soka ya Uingereza.

Katika mechi ya kwanza, Fernandes na Pogba walichezeshwa pamoja na Man-United kupoteza mchuano huo kwa mabao 2-1.

Fernandes ambaye ni mzawa wa Ureno, aliwafungia Man-United kupitia mkwaju wa penalti kabla ya kupoteza penalti ya pili mwishoni mwa kipindi cha pili.

Hata hivyo, Man-United walirejea kwa matao ya juu katika mechi ya pili na kusajili ushindi wa 3-1.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer amedokeza uwezekano wa kupanga Fernandes na Pogba katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) utakaowakutanisha na Tottenham Hotspur ugenini mnamo Juni 19, 2020. Mechi hiyo itafufua vita vya kuwania nafasi ya kuingia ndani ya mduara wa nne-bora na hatimaye kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Solskjaer amekiri kwamba ushirikiano kati ya Pogba, Fernandes, Anthony Martial, Mason Greenwood, Daniel James na Timothy Fosu-Mensah katika mechi ya kwanza ya kirafiki dhidi ya West Brom ulimridhisha zaidi licha ya kwamba kikosi chake kilizidiwa nguvu.

Wanasoka waliotegemewa zaidi na Man-United katika mechi ya pili ni Marcus Rashford, Harry Maguire, David De Gea, Victor Lindelof na Odion Ighalo aliyerefusha mkataba wake majuzi hadi Januari 2021.

Wachezaji wa Man-United walicheza wao kwa wao mwanzoni mwa wiki hii baada ya mechi ya kirafiki iliyokuwa iwakutanishe na Stoke City kufutiliwa mbali kufuatia tukio la kocha Michael O’Neill kupatikana na virusi vya homa kali ya corona.

Kwa upande mwingine, Tottenham waliokuwa wakijivunia huduma za Harry Kane, Son Heung-min Erik Lamela walipoteza tena dhidi ya Norwich City katika uwanja wao wa nyumbani baada ya kutandikwa 2-1 katika mechi ya kirafiki iliyowakutanisha Juni 12, 2020.

Tottenham waliwahi kuzidiwa maarifa na Norwich almaarufu ‘The Canaries’ katika mechi ya Carabao Cup mnamo Machi. Kushindwa huko kulishuhudia wanasoka wa Tottenham wakizomewa na mashabiki, tukio ambalo lilizua makabiliano makali uwanjani kati ya mmoja wao na beki Eric Dier.