CAF: Gor yaorodhesha sababu za kubanduliwa na USM Alger
Na Geoffrey Anene
MASHABIKI wa Gor Mahia wamelaumu mrundiko wa mechi nyingi na kuuzwa kwa wachezaji nyota Meddie Kagere na Godfrey Walusimbi kwa masaibu ya timu hiyo kubanduliwa nje ya Kombe la Mashirikisho la Afrika mwaka 2018 baada ya kuliwa 2-1 na USM Alger nchini Algeria, Jumatano.
Mshambuliaji wa Congo Brazzaville Prince Ibara na Amir Sayoud walifungia USM Alger dakika ya 38 na 82 mtawalia kabla ya mvamizi kutoka Rwanda Jacques Tuyisenge kupachika bao la Gor kufutia machozi dakika ya 83.
Baada ya mchuano huu wa mwisho wa Kundi D, mashabiki walijitosa kwenye mitandao ya kijamii kutoa maoni yao, wengi wakiamini Gor ingesalia mashindanoni kama ratiba ya mechi za ligi ingekuwa nzuri na pia viongozi wa klabu wangewakwamilia raia wa Rwanda Kagere na Mganda Walusimbi.
Shabiki Kano Clans Kisumu alipongeza kocha Dylan Kerr na vijana wake kabla ya kuongeza, “Mechi nyingi katika muda mfupi pamoja na kuuzwa kwa Kagere na Walusimbi kulichangia pakubwa katika kuondolewa kwetu mashindanoni.” Mashabiki wengi wana maoni sawa na haya.
Naye Abdul Wahab anaamini Gor inastahili kujilaumu yenyewe. “Gor ilikuwa na fursa nzuri sana dhidi ya Rayon Sports, na cha kushangaza ikaitupa. Kubanduliwa nje ni adhabu ambayo sisi wenyewe tulijitakia. Katika soka, usipotumia nafasi zako vyema, unaishia kujuta. Napenga Gor Mahia, lakini hakuna njia tungeweza kushinda USM Alger kwao na kuwabandua nje…,” alisema.
Jimson Omondison alielekeza hasira yake kwa viongozi wa Gor Mahia. “(Ambrose) Rachier unafurahia sasa matokeo haya…hatuelewi kilichokufanya ukaachilia Walusimbi ahamie Afrika Kusini, tafadhali tueleze kiasi cha fedha ulichomuuza. Tunaumia. Kama mashabiki tunataka ujiandae kutupa sababu muhimu sisi kubanduliwa nje.
Usilaumu KPL (kampuni inayoendesha Ligi Kuu nchini Kenya) kuhusu mrundiko wa mechi, umeshindwa kudhibiti wachezaji….” Mashabiki wengi wameridhishwa na umbali Gor ilifika na kuomba viongozi wa klabu kutafuta mshambuliaji na pia kutoachilia wachezaji kuondoka katikati ya msimu. Wameitaka Gor iangazie msimu ujao badala ya kujihurumia.
USM Alger ilishinda kundi hili kwa alama 11 nayo Rayon ikanyakua tiketi ya mwisho ya robo-fainali baada ya kupapura Young Africans (Yanga) kutoka Tanzania 1-0 jijini Kigali, Rwanda. Gor ilikamilisha kampeni yake katika nafasi ya tatu katika kundi hili kwa alama nane nayo Yanga ikavuta mkia kwa alama nne.