Michezo

Caleb achaguliwa mwenyekiti FKF Nairobi Magharibi, Maureen Obonyo awakilisha jinsia ya kike

September 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

CALEB Ayodi Malweyi amechaguliwa mwenyekiti mpya kuongoza Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Tawi la Nairobi Magharibi ndani ya muhula wa miaka minne ijayo.

Uchaguzi huo uliandaliwa katika Uwanja wa Ligi Ndogo Ngong Road, Nairobi.

Caleb na naibu wake, Alfred Mutua Muli walishinda wadhifa huo kwa kuzoa kura 53 dhidi ya kura tatu za Charles Ng’ang’a Njoroge na mgombea mwenza Wilfred Marori Mokaya.

Caleb Ayodi Malweyi na Alfred Mutua Muli (mwenyekiti na naibu wake mtawalia) wa FKF Tawi la Nairobi Magharibi wakihojiwa baada ya kutangazwa washindi. Picha/ John Kimwere

”Kwanza nashukuru wajumbe wote kwa kuonyesha wana imani nami kuongoza tawi la Nairobi Magharibi kwenye jitihada za kukuza soka ndani ya miaka minne ijayo,” Caleb alisema na kutoa mwito kwa viongozi wa klabu za eneo hilo kusaidiana kukuza mchezo huo wa soka.

Naye Hannington Khayati alichaguliwa mwakilishi wa vijana kwa kura 55 huku mpinzani wake Moses Were akipata zero.

Kwenye wadhifa wa katibu, Charles Kioko Kaindi alizoa kura 51 huku Martin Karanja akipata nne.

Nao Maureen Obonyo na Josphat Karuri walihifadhi nyadhifa zao kama mwakilishi wa wanawake na mwekahazina waliposhinda Susan Mudongoi na Meshack Onchonga mtawalia.

Kwingineko Katika Tawi la Laikipia Abdul Kaka alichaguliwa mwenyekiti mpya kwa kura nne dhidi ya kura tatu za Francis Kibe. Katika tawi la Nairobi Mashariki Amos Otieno alichaguliwa mwenyekiti mpya aliposhinda kwa kura 51 dhidi ya 45 za George Onyango aliyekuwa naibu mwenyekiti muhula uliopita.