Casillas ajiondoa kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Uhispania
Na CHRIS ADUNGO
ALIYEKUWA kipa na nahodha wa timu ya taifa ya Uhispania, Iker Casillas amejiondoa katika kivumbi cha kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF).
Mlinda-lango huyo wa zamani wa Real Madrid amesema kujiondoa kwake kumechochewa na hali mbali ya sasa inayotishia maendeleo ya Uhispania kijamii, kiuchumi na kiafya tangu kulipuka kwa virusi vya homa kali ya corona.
Hadi kufikia Juni 17, zaidi ya watu 27,000 walikuwa wameaga dunia nchini Uhispania kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
“Ripoti hizi ni za kuvunja moyo. Sioni tija na fahari yoyote kuwania kiti hiki wakati ambapo taifa linalopitia changamoto nyingi za kila sampuli,” akasema Casillas, 39.
Ingawa Casillas hajatangaza kustaafu rasmi kwenye ulingo wa usogora, kipa huyo hawajawahi kuwajibishwa na waajiri wake FC Porto nchini Ureno katika mchuano wowote tangu Aprili 2019 alipopata mshutuko wa moyo akishiriki mazoezi.
Baada ya kupona, alipokezwa baadhi ya majukumu katika benchi ya kiufundi ya Porto mnamo Julai 2019.
Kujiondoa kwa Casillas kunamsaza Rais wa sasa wa RFEF, Luis Rubiales katika nafasi maridhawa ya kuchaguliwa tena bila kupingwa kwa muhula mpya wa miaka minne katika uchaguzi utakaoandaliwa mnamo Agosti 2020.