Cecafa yatangaza ratiba ya mechi za 2019
Na GEOFFREY ANENE
BARAZA la Mashirikisho ya Soka ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetangaza ratiba ya mashindano yake ya mwaka 2019.
Wafalme wa soka ya wanaume, Kenya, ambao walijiondoa kuwa wenyeji wa Senior Challenge Cup mwaka 2018, wataandaa soka ya Challenge Cup ya wanawake pekee. Tarehe za Challenge Cup ya wanawake bado hazijatangazwa.
Hata hivyo, tarehe za kuanza mashindano mengine sita zimetangazwa. Mashindano hayo ni Kagame Cup yanayokutanisha mabingwa ligi wa mataifa husika, Wavulana wasiozidi umri wa miaka 17, wanaume wasiozidi umri wa miaka 20, wanawake wasiozidi umri wa miaka 20, Challenge Cup ya Wanawake na Senior Challenge Cup.
Cecafa ilitangaza wenyeji na tarehe za mashindano haya ilipokutana jijini Addis Ababa nchini Ethiopia siku chache zilizopita katika mkutano uliohudhuriwa na maafisa kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) akiwemo Rais Gianni Infantino na wale kutoka Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) ikiongozwa na Ahmad Ahmad.
Kalenda ya Cecafa inatarajiwa kuanza mwezi Juni kwa hivyo huenda Kenya ikawa mwenyeji wa Challenge Cup ya wanawake mwezi huo ama mwezi Oktoba, miezi ambayo haina mashindano ya Cecafa.
FIFA itadhamini U-17 Challenge Cup (Wavulana/Eritrea), U-17 Challenge Cup (Wasichana/Kenya), U-20 Challenge Cup (Wanawake/Uganda), Senior Challenge Cup (Wanawake/Tanzania) na U-20 Challenge Cup (Wanaume/Uganda).
Mashindano ya Kagame Cup na Senior Challenge Cup yanafadhiliwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame na kampuni ya Azam kutoka Tanzania, mtawalia. Wanachama wa Cecafa ni Uganda, Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi, Zanzibar, Sudan Kusini, Sudan, Somalia, Djibouti, Eritrea na Ethiopia.
Ratiba ya Cecafa (2019):
Julai/Agosti
Soka ya Kagame Cup (Rwanda)
Agosti
Soka ya Wavulana ya Under-17 (Eritrea)
Septemba
Soka ya Wavulana ya Under-20 (Uganda)
Novemba
Soka ya Challenge Cup ya Wanawake (Tanzania)
Desemba 1-16
Soka ya Senior Challenge Cup (Uganda)