Michezo

Celtic wanyanyua ufalme wa Scottish Cup kwa mara ya 40

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

CELTIC waliwapokeza Hearts kichapo cha 4-3 kupitia penalti na kutwaa taji la Scottish Cup kwa mara ya 40 mnamo Jumapili ya Disemba 20, 2020.

Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia penalti baada ya vikosi vyote kutoshana nguvu kwa sare ya 3-3 mwishoni mwa muda wa ziada.

Kristoffer Ajer alifungia Celtic penalti ya mwisho na kusaidia waajiri wake kunyanyua taji lililoanza kuwaniwa na vikosi vya Scotland katika msimu wa 2019-20 kabla ya kukamilika baada ya miezi 16 kwa kuwa kivumbi hicho kiliahirishwa kwa sababu ya corona.

Ryan Christie na Odsonne Edouard waliwaweka Celtic kifua mbele kwa mabao 2-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza kabla ya Liam Boyce na Stephen Kingsley kusawazishia Hearts na kufanya kivumbi hicho kuingia muda wa ziada.

Japo Leigh Griffiths aliwarejesha Celtic uongoni katika dakika ya 105, jitihada zake zilifutwa na Josh Ginnelly aliyefanya mchuano kuingia kwenye penalti ndipo mshindi apatikane.

Kabla ya kupigwa kwa fainali hiyo, kocha Neil Lennon alikuwa na presha ya kutimuliwa baada ya mashabiki kuanza kuandamana nje ya uwanja kutokana na msururu wa matokeo duni yaliyoshuhudia kikosi hicho kikipiga msururu wa michuano mitano bila ya kusajili ushindi wowote.

Hearts, walioshushwa ngazi katika Ligi Kuu ya Scotland mnamo Machi baada ya kivumbi hicho kusitishwa ghafla mnamo Machi, walijibwaga ugani dhidi ya Celtic wakijivunia uongozi wa jedwali la Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship).

Ingawa walikuwa wakipigiwa upatu wa kutwaa taji la Scottish Cup kwa mara ya tisa mfululizo, kikosi hicho kilipokezwa kichapo cha tisa mfululizo kutoka kwa Celtic walio na makao yao makuu jijini Glasgow.

Celtic kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa Ross County katika mechi ya Ligi Kuu mnamo Disemba 23 huku Hearts wakitarajiwa kushuka dimbani kuvaana na Ayr katika kipute cha Championship mnamo Disemba 26.