Michezo

Chapa Dimba yasaidia kijana kutimiza ndoto

December 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JEFF KINYANJUI na GEOFFREY ANENE

KIJANA Abdalla Maro wa klabu ya Berlin FC ya Garissa aliibuka mfungaji bora wa mabao katika kabumbu ya Chapa Dimba na Safaricon kanda ya Kaskazini Mashariki.

Kutokana na kiwango chake cha juu katika usakataji soka, kadhalika mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 17 amejumuishwa kwenye timu ya vijana itakayozuru Uhispania mwaka ujao kwa mazoezi ya siku 10 katika vituo vya kunoa vipaji vya LaLiga.

Ni ndoto iliyotimia kwa kijana huyo baada ya kukosa nafasi hiyo mwaka uliopita kutokana na matatizo ya stakabadhi za usafiri.

“Nilichaguliwa mwaka uliopita, lakini nikakosa vyeti muhimu vya usafiri. Raundi hii, nina kila kitu na tayari kabisa kwa safari,” Abdalla aliyefunga mabao matatu katika mashindano hayo alisema.

Abdalla ni shabiki mkubwa wa klabu ya Real Madrid na anaamini ziara hii itafungua milango yake ya kucheza soka ya kulipwa.

“Nilianza kucheza soka nikiwa na umri mdogo na sijawahi kurudi nyuma kamwe. Nina hakika kupitia kwa Chapa Dimba nitapata fursa ya kuvutia maskauti ambao watanitafutia klabu ya kuchezea barani Ulaya. Kusakata soka ndiyo kazi ninayotaka kufanya maishani mwangu. Naipongeza Safaricom kwa kunitambua na kunipa nafasi hii itakayoniwezesha kufaulisha ndoto yangu ya muda mrefu,” aliongeza.

Baada ya mechi za kufana eneo la Kaskazini Mashariki, michuano ya Chapa Dimba na Safaricom imehamia Pwani ambapo fainali zitafanyika uwanjani Bomu mwishoni mwa wiki hii.

Uwanja huo, kadhalika utatumika kwa fainali za hapo Juni huku Abdalla akitarajia kuisaidia klabu yake ya Berlin kutwaa ubingwa.

“Lengo letu ni kutwaa ubingwa wa kitaifa na tunajiandaa vikali kutimiza ndoto hiyo. Tungependa kuhakikishia ulimwengu kwamba hata Kasakazini Mashariki mwa Kenya kuna vipaji vya hali ya juu licha ya eneo hilo kupuuzwa kwa muda mrefu.”

Berlin FC sasa ni mabingwa mara mbili wa Chapa Dimba na Safaricom eneo la Kaskazini Mashariki.

Yahya Muhamud aliibuka kipa bora naye Noor Osman akatawazwa mchezaji bora wa Chapa Dimba na Safaricom katika mashindano hayo ya Kaskazini Mashariki.

Aidha, mashindano haya yataelekea eneo la Pwani wikendi hii. Uwanja wa Bomu mtaani Changamwe mjini Mombasa utatumiwa kwa fainali za Pwani.