Charlie Austin aponyoka adhabu ya FA
NA CECIL ODONGO
MSHAMBULIZI wa Southampton Charlie Austin ameepuka pembamba adhabu kali ya Shirikisho la soka nchini Uingereza FA baada ya kulalamikia hatua ya refa wa mechi kufutilia mbali bao lao dhidi ya Watford siku ya Jumamosi na kuitaja kama ‘mzaha mkubwa’.
Manolo Gabbiadini aliwaweka ‘The Saints’ mbele kupitia bao safi kipindi cha kwanza kwenye uga wao wa nyumbani wa St. Mary kabla ya Austin kufunga la pili kipindi cha pili ila refa Simon Hooper baada ya mashauriano na msaidizi wake Harry Lennard, alifutilia mbali bao hilo kwa imani kwamba mlinzi Maya Yoshinda alikiwa ameotea alipojaza mpira wavuni mbele ya mlinda lango Ben Foster.
“Ni jambao la mzaha na hawakufaa kupata sare hii. Tulifunga bao safi na kuwa kifua mbele kwa mabao 2-0 lakini wasimamizi wa mechi walitunyima ushindi wa wazi kwa kukataa bao letu,” akasema Austin baada ya mechi hiyo.
Sheria za FA zinaonyesha wazi kwamba mchezaji na makocha hawafai kuwashutumu wasimamizi wa mechi kupitia matamshi yasiyofaa ila tamko la Austin limechukuliwa kama la wastani na lisilovutia adhabu kali.