Chebet, Moraa na Krop watang’aa Zurich Diamond League, Yego avuta mkia
WATIMKAJI Beatrice Chebet (mita 5,000), Mary Moraa (800m) na Jacob Krop (3,000m) waliachia vumbi wapinzani wao katika riadha za Diamond League mjini Zurich nchini Uswisi mnamo Alhamisi usiku, Septemba 5, 2024.
Bingwa wa Olimpiki wa 5,000m na 10,000m, Chebet alilenga kufuta rekodi ya dunia ya Muethiopia Gudaf Tsegay (14:00.21).
Ingawa hakufanikiwa kuweka rekodi mpya ya dunia, Chebet alinyakua taji la 5,000m kwa kukamilisha mizunguko hiyo 12 na nusu kwa rekodi ya Zurich Diamond League ya dakika 14:09.52.
Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alifuta rekodi ya Mkenya mwenzake Vivian Cheruiyot ya 14:30.10 iliyowekwa Septemba 8, 2011.
Pia, Chebet aliimarisha muda bora mwaka huu wa 14:18.76 ambao Muethiopia Tsigie Gebreselama alikuwa ameandikisha mwezi Mei 2024 mjini Eugene, Amerika.
Chebet alifuatwa kwa karibu na Waethiopia Ejgayehu Taye (14:28.76) na Gebreselama (14:39.05), mtawalia.
Mkenya mwingine katika kitengo hicho, Margaret Akidor alikamata nafasi ya 10 kwa 14:55.67.
Bingwa wa Jumuiya ya Madola na dunia wa 800m, Moraa alibeba taji la mbio hizo za kuzunguka uwanja mara mbili kwa dakika 1:57.08 akifuatiwa na Muingereza Goergia Bell (1:57.94) na Addison Wiley kutoka Amerika (1:58.16).
Krop naye aliongoza Mkenya mwenzake Cornelius Kemboi kufagia nafasi mbili za kwanza kwa dakika 7:34.80 na 7:35.46, huku Mbelgiji Isaac Kimeli aliyezaliwa Kenya, akifunga tatu-bora (7:41.30).
Mkenya Daniel Munguti hakumaliza mbio baada ya kujiondoa ikisalia mita 1,000.
Mabingwa wa zamani wa dunia Reynold Cheruiyot (chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20) na Timothy Cheruiyot (watu wazima) pamoja na Boaz Kiprugut walisikitisha katika mbio za 1,500m walizokamilisha katika nafasi ya sita, 11 na 14, mtawalia.
Bingwa wa Afrika Julius Yego pia hakuwa na lake mjini Zurich baada ya kuvuta mkia katika urushaji mkuki. Aliandikisha mtupo wa mita 69.61.
Nafasi tatu za kwanza ziliwaendea Anderson Peters kutoka Grenada (85.72m), Mjerumani Julian Weber (85.33) na Mjapani Genki Dean Roderick (82.69), mtawalia.