• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Chelsea wamsajili kipa raia wa Senegal kutoka Rennes

Chelsea wamsajili kipa raia wa Senegal kutoka Rennes

Na MASHIRIKA

CHELSEA wamemsajili kipa Edouard Mendy kutoka Rennes ya Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitano.

Mlinda-lango huyo raia wa Senegal, 28, aliwajibishwa mara 25 na Rennes katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) tangu aingie katika sajili rasmi ya kikosi hicho baada ya kuagana na Reims ya Ufaransa mnamo 2019.

Mendy alifanyiwa vipimo vya afya mnamo Septemba 22, 2020 na ujio wake unatazamiwa kutoa presha zaidi kwa kipa ghali Kepa Arrizabalaga aliyesajiliwa na Chelsea kwa kima cha Sh9.9 bilioni kutoka Athletic Bilbao.

“Nina furaha tele kujiunga na Chelsea. Hiki ni kikosi ambacho nimekuwa na ndoto ya kukichezea tangu utotoni,” akasema Mendy.

Masihara ya Kepa yalichangia bao la pili lililofungwa na fowadi Sadio Mane katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na Liverpool dhidi ya Chelsea katika gozi la Ligi Kuu ya Uingeeza (EPL) mnamo Agosti 20, 2020 uwanjani Stamford Bridge.

Awali, kusuasua kwa kipa huyo kulichangia bao jingine lililofungwa na Brighton katika mechi ya ufunguzi wa msimu huu uwanjani Amex mnamo Septemba 14. Chelsea walisajili ushindi wa 3-1 katika mchuano huo.

Matokeo duni ya Kepa ambaye ni raia wa Uhispania katika mechi muhimu ni kiini cha kocha Frank Lampard kumtema katika kikosi cha kwanza cha Chelsea msimu uliopita wa 2019-20.

Mojawapo ya mechi hizo ni ile ya fainali ya nusu-fainali ya Kombe la FA iliyoshuhudia nafasi ya Kepa, 25, ikitwaliwa na kipa mkongwe, Willy Caballero, 38.

Baada ya Chelsea kuzabwa na Liverpool, Lampard alisema kwamba Caballero ndiye ataunga kikosi cha kwanza katika mechi ya Carabao Cup itakayowakutanisha na Barnsley uwanjani Stamford Bridge mnamo Septemba 22.

“Kepa lazima ajitahidi na nitajitolea kumsaidia. Katika kiwango cha mtu binafsi, kila mchezaji huhitaji usaidizi na uungwaji mkono. Lazima tujikakamue kumfaa ili aanze kujiamini kwa sababu hilo ndilo muhimu zaidi,” akasema Lampard ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Chelsea.

Msimu uliopita, Mendy hakufungwa katika mechi tisa kati ya 24 za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ikilinganishwa na rekodi ya Kepa ambaye hakufungwa bao katika mechi nane pekee kati ya 33 za EPL.

Ina maana kwamba Mendy aliokoa asilimia 76.3 ya mabao na akafungwa goli kila baada ya dakika 114. Kwa upande wake, Kepa aliokoa asilimia 53.5 ya mabao huku akifungwa goli kila baada ya dakika 63.

Hata hivyo, Kepa alipiga asilimia 79.7 ya pasi ikilinganishwa na asilimia 70.1 ya Mendy.

Mendy amechezea timu ya taifa ya Senegal mara nane na anakuwa sasa mwanasoka wa nane kusajiliwa na Chelsea hadi kufikia sasa msimu huu.

Anafuata nyayo za kipa wa zamani wa Chelsea, Petr Cech aliyetua ugani Stamford Bridge kutoka Rennes mnamo 2004. Cech ambaye pia amewahi kudakia Arsenal, sasa ni mkurugenzi wa kiufundi kambini mwa Chelsea na mshauri wa makipa.

“Cech alipomtambua Edouard na ombi lake kuidhinishwa na benchi nzima ya kiufundi, hatukusalia na jingine la kufanya ila kumsajili kipa huyo ambaye anajiunga nasi wakati ambapo tunamhitaji zaidi,” akasema mkurugenzi wa Chelsea, Marina Granovskaia.

  • Tags

You can share this post!

Di Maria kukosa mechi nne kwa utovu wa nidhamu

Winga chipukizi wa Kangemi alenga kufikia upeo wa Mohamed...