Chelsea wapepeta Manchester United 3-1 kujikatia tiketi ya kuvaana na Arsenal fainali ya FA
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Frank Lampard amefichua kwamba kubwa zaidi katika maazimio ya Chelsea kwa sasa ni kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kutia kapuni ubingwa wa Kombe la FA.
Hii ni baada ya Chelsea kuwapepeta Manchester United 3-1 katika nusu-fainali ya Kombe la FA mnamo Julai 19 uwanjani Wembley, Uingereza.
Ushindi huo wa Chelsea ambao walitamalaki mpira na kuwazidi maarifa wapinzani wao katika takriban kila idara, ulikomesha rekodi ya kutoshindwa kwa Man-United katika msururu wa mechi 19 za awali katika mapambano yote.
Fowadi Olivier Giroud aliwafungulia Chelsea ukurasa wa mabao mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya chipukizi Mason Mount kufunga la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Presha ya washambuliaji wa Chelsea kwa Man-United ilichangia beki Harry Maguire kujifunga kunako dakika ya 74 kabla ya kiungo Bruno Fernandes kuwafungia Man-United penalty dakika tano kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa rasmi.
Mabao mawili ya kwanza ya Chelsea yalitokana na masihara ya kipa David De Gea ambaye kocha Ole Gunnar Solskjaer alimwaminia kujaza nafasi ya mlinda-lango Sergio Romero ambaye hadi kufikia nusu-fainali, alikuwa tegemeo la kikosi cha kwanza cha Man-United katika michuano ya Kombe la FA msimu huu.
Chelsea kwa sasa watakutana na Arsenal kwenye fainali itakayoandaliwa uwanjani Wembley mnamo Agosti 1. Arsenal ambao ni mabingwa mara 13 wa Kombe la FA walitinga fainali ya kivumbi hicho msimu huu baada ya kuwapepeta washikilizi Machester City 2-0 mnamo Julai 18 kupitia mabao ya Pierre-Emerick Aubameyang.
“Sasa nalenga kutia kapuni Kombe la FA kwa mara ya tano kitaaluma nitakapowaongoza Chelsea kuvaana na Arsenal kwenye fainali. Naamini itakuwa mechi ya kukata na shoka dhidi ya waajiri wangu wa zamani. Itakuwa ni mechi spesheli sana kwangu,” akasema Giroud.