Michezo

Chelsea yaadhibiwa kwa kukosa nidhamu uwanjani

May 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

CHELSEA imepigwa faini ya Sh2, 716,057 na Shirikisho la Soka nchini Uingereza (FA) kwa utovu wa nidhamu.

Wachezaji na makocha walifanya kosa la kuzingira refa na kumfokea wakati wa mapumziko wa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Huddersfield iliyomalizika 1-1 Mei 9, 2018.

‘The Blues’ walikasirishwa na uamuzi wa refa Lee Mason kuwapa kona, lakini kabla ya Willian kuipiga, akapuliza kipenga cha kukamilisha dakika hizo 45 za kwanza. Afisa huyu aliamua kwamba kipindi cha kwanza kilikuwa kimetamatika.

Nahodha Cesar Azpilicueta, kiungo Cesc Fabregas na beki Antonio Rudiger waliongoza katika kumchemkia Mason. Kocha msaidizi Carlo Cudini aliondoa Rudiger karibu na refa huyo kwa kumvuta. Cudini pia aliongelesha Mason.

“Chelsea imepigwa faini ya Sh2, 716,057 baada ya kukubali kosa la kushindwa kuhakikisha wachezaji na maafisa wake wanaonyesha mfano mwema,” taarifa kutoka FA ilisema.

Chelsea ilikashifu Huddersfield kwa kupoteza muda wakati wa mechi hiyo, matokeo yaliyozima matumaini yake ya kuingia Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao. Kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Newcastle katika siku ya mwisho ya Ligi Kuu ya Uingereza hapo Mei 13 kilihakikisha Chelsea inakamilisha katika nafasi ya tano.

Chelsea ya kocha Antonio Conte inaweza kumaliza msimu na taji ikiwa itafaulu kulemea Manchester United ya kocha Jose Mourinho katika fainali ya Kombe la FA hapo Mei 19 uwanjani Wembley.