Michezo

Chepkoech aongoza watatu kuingia Riadha za Dunia mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji

September 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Beatrice Chepkoech alishinda kwa urahisi kitengo chake kwenye mashindano ya kuchagua timu itakayowakilisha Kenya katika Riadha za Dunia zitakazofanyika jijini Doha nchini Qatar mnamo Septemba 27 hadi Oktoba 6, 2019.

Katika mchujo huo wa kitaifa ulioanza uwanjani Nyayo jijini Nairobi mnamo Septemba 12, malkia huyo wa Riadha za Diamond League alidhihirisha uweledi wake kutoka mwanzo na kukamilisha mizunguko hiyo 28 na kuruka maji mara saba kwa dakika 9:45.15.

Muda huu, hata hivyo, ni kasi ya kobe ukilinganisha na rekodi yake ya 8:44.32 aliyoweka mjini Monaco mwezi Julai mwaka 2018.

Alifuatiwa kwa karibu na bingwa wa dunia mwaka 2015 Hyvin Kiyeng (9:45.20), mshindi mara mbili wa mataji ya dunia ya mbio za wakimbiaji wasiozidi umri wa miaka 20 Celliphine Chespol (9:45.24) naye bingwa wa Olimpiki ya chipukizi Fancy Cherono akafunga mduara wa nne-bora.

Kenya inaruhusiwa kuwa na wakimbiaji wanne katika kitengo hiki kwa sababu Chepkoech alishinda Diamond League.

Katika matokeo mengine katika siku ya kwanza, malkia wa mbio za mita 400 wa michezo ya Afrika (African Games), Vanice Kerubo alitwaa taji kwa sekunde 59.66.

Hata hivyo, muda wake ni nje ya ule wa kushindana jijini Doha wa sekunde 56.00.

Naye Michael Kibet aliduwaza wakimbiaji 21 wakiwemo mastaa Bethwell Birgen, Richard Yator, Rhonex Kipruto, Ronald Kwemoi, Edward Zakayo na wengineo akishinda mbio za mita 5,000.

Kibet alimzima mpinzani wake wa karibu Daniel Simiyu katika mita 100 za mwisho akinyakua tiketi kwa dakika 13:26.83. Simiyu (13:27.95) na Nicholas Kimeli (13:29.99) waliridhika katika nafasi ya pili na tatu, mtawalia.

Mbio za mita 800 

Baadhi ya mbio zinazotarajiwa kusisimua katika siku ya pili na mwisho hapo Ijumaa ni mbio za mita 800.

Eglay Nalianya alitinga fainali baada ya kushinda mchujo wa kwanza wa mbio za mita 800 kwa dakika 2:03.60 akifuatiwa kwa karibu na Jarinta Mawia naye Emily Tuwei alitawala mchujo wa pili kwa 2:04.74.

Bingwa wa dunia mwaka 2013 Eunice Sum alifuata Tuwei naye Jackline Wambui akamaliza wa tatu.

Katika kitengo cha wanaume, bingwa wa Diamond League mwaka 2018 Emmanuel Korir alishinda nusu-fainali ya kwanza akifuatwa unyounyo na Abel Kipsang na Ferguson Rotich naye Edward Kemboi akatawala nusu-fainali ya pili mbele ya Jonathan Kitilit second na Kipng’etich Ng’eno.