Chipu sasa pua na mdomo kupata kocha mpya – KRU
Na CHRIS ADUNGO
WANARAGA chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 almaarufu Chipu sasa watapata kocha mpya mwishoni mwa mwezi huu wa Desemba.
Haya ni kwa mujibu wa Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), Thomas Odundo ambaye amekiri kwamba mchakato wa kutafuta mkufunzi wa kikosi hicho unaelekea kukamilika.
Katika mahojiano yake na Taifa Leo, Odundo amethibitisha kwamba jumla ya wakufunzi 19 (tisa wa humu nchini na raia 10 wa mataifa ya kigeni) walituma maombi ya kuzingatiwa kwa kazi ya kudhibiti mikoba ya Chipu.
Mdokezi wetu katika KRU amesema kwamba huenda wakalazimika kuendea huduma za mkufunzi wa humu nchini kwa sababu ya changamoto za kifedha ambazo shirikisho linapitia kutokana na janga la corona.
Hata hivyo, Paul Murunga ambaye ni kocha wa zamani wa Chipu na Kenya Sevens almaarufu Shujaa ndiye anapigiwa upatu zaidi kupokezwa mikoba ya makinda hao.
“Mshindi atafichuliwa rasmi na KRU mwishoni mwa mwezi huu. Mahojiano yako pua na mdomo kukamilika na yamekuwa yakiendeshwa kupitia mtandaoni,” akasema Odundo.
“Murunga amewahi kuwa na kikosi cha Chipu na anaelewa ukubwa wa matarajio ya KRU, mashabiki na wadau wengine wa mchezo huo. Ana tajriba pevu na uzoefu mpana,” akasema mdokezi wetu.
Murunga, Mitch Ocholla na Dominique Habimana ndio walikuwa wawaniaji wakuu wa mikoba ya Chipu iliyosalia bila mkufunzi baada ya Paul Odera kupokezwa majukumu ya kutia makali wanaraga wa Kenya Simbas.
KRU ilianza mchakato wa kutafuta kocha mpya wa Chipu mnamo Septemba 28 ilipotangaza kuwa inatafuta mkufunzi aliyehitimu kiwango cha pili cha ukufunzi wa kimataifa (World Rugby Level Two Certificate) katika kikosi cha wanaraga saba au 15 kila upande kwa mujibu wa viwango vya Raga ya Dunia (WR).
Murunga aliwahi kuwanoa vijana wa Chipu kwa miaka minne na kuwaongoza kufuzu kwa Olimpiki za Chipukizi zilizoandaliwa nchini China mnamo 2015.
Isitoshe, mkufunzi huyo wa zamani wa Homeboyz ndiye aliyekuwa msaidizi wa kocha Benjamin Ayimba wakati Shujaa walipotwaa taji la Singapore Sevens kwenye kampeni za Raga ya Dunia mnamo 2016.
Murunga alikuwa pia sehemu ya maafisa wa benchi ya kiufundi walioongoza Shujaa kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki iliyoandaliwa jijini Rio, Brazil mnamo 2016. Aliaminiwa kuwa kocha mkuu wa Shujaa mnamo 2018-19 baada ya Simiyu kujiuzulu.
Kibarua cha kwanza kinachomkabili kocha mpya wa Chipu ni kuongoza kikosi hicho kuhifadhi Kombe la Afrika kwa Chipukizi, Barthes Trophy. Kwa mwaka wa pili mfululizo, mshindi wa taji hilo atafuzu kwa raga ya dunia ya Junior Rugby World Trophy.
Kivumbi cha Barthes Trophy kilikuwa kiandaliwe jijini Nairobi kati ya Aprili 19-26, kabla ya kuahirishwa hadi mwakani kwa sababu ya janga la corona. Kenya imetiwa katika zizi moja na Zambia, Tunisia na Bukini.
Chini ya Odera, Chipu iliwaduwaza wapambe wa Afrika, Namibia kwa alama 21-18 katika fainali ya Barthes Cup 2019 iliyochezewa Ruaraka na kufuzu kwa Raga ya Dunia (JWRT) nchini Brazil. Walipepeta wenyeji Brazil 26-24, wakapokezwa na Uruguay kichapo cha 63-11 na kucharazwa na 48-34 na Japan walioibuka kileleni mwa kundi.
Kwa mujibu wa Odundo, kubwa zaidi katika matamanio ya Chipu ni kufuzu kwa kivumbi cha JWRT kwa mara ya pili mfululizo mnamo 2021 kabla ya Kenya kuwa mwenyeji wa fainali hizo mnamo 2024. Kenya italazimika kuzamisha chombo cha Colombia katika mchujo ili kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.