Chipu sokoni kutafuta kocha Murunga, Ocholla na Habimana wakipigiwa upatu
Na GEOFFREY ANENE
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa, Paul Murunga anapigiwa upatu kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya chipukizi, licha ya kuwa zoezi la kutafuta kocha limeanza tu.
Shirikisho la Raga Kenya (KRU) lilitangaza Septemba 28 kuwa linatafuta kocha mpya wa Chipu baada ya aliyekuwa mshikilizi wa wadhifa huo, Paul Odera “Paul O” kupandishwa madaraka kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya watu wazima almaarufu Simbas mwezi Mei 31, 2019. Odera amekuwa pia akiongoza Chipu kwa zaidi ya miaka mitano.
Wanaotaka kuajiriwa kuongoza Chipu wamepewa hadi Oktoba 10 kutuma maombi yao kwa KRU.
Murunga aliwahi kuwa kocha wa Chipu kabla ya Odera kutwikwa majukumu hayo. Pau, jinsi Murunga anafahamika kwa jina la utani, pia alipata umaarufu mkubwa akiwa kocha wa klabu ya Homeboyz.
Isitoshe, Murunga aliwahi kuhudumu kama naibu wa kocha katika timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa chini ya Benjamin Ayimba kabla ya kuwa kocha mkuu wa timu hiyo msimu 2018-2019 akichukua hatamu ya uongozi kutoka kwa Innocent ‘Namcos’ Simiyu.
Mbali na Murunga, duru za kuaminika zinasema kuwa makocha wa zamani wa klabu ya raga ya Nakuru Dominique Habimana na Mitch Ocholla pia wanaweza kupokezwa mikoba ya ukocha ya Chipu kwa sababu wana ujuzi wa miaka mingi na wamefuzu na viwango vya ukocha ambavyo KRU inatafuta.
Kocha wa Impala Saracens Ocholla, ambaye aliwahi kunoa Chuo Kikuu cha Strathmore, aliongoza timu ya Shujaa msimu 2010-2012.
Mzawa wa Rwanda, Habimana, ambaye ana uraia wa Kenya baada ya kuishi humu nchini kwa zaidi ya miaka 30, aling’atuka kutoka cheo cha kocha mkuu wa klabu ya Kenya Harlequin mwisho wa msimu 2019-2020 baada ya kuwa nayo msimu mmoja. Habimana aliwahi kuhudumu kama mmoja wa manaibu wa kocha mkuu wa timu ya Kenya Simbas chini ya kocha kutoka Afrika Kusini Jerome Paarwater.
Jukumu la kwanza kubwa ambalo kocha mpya wa Chipu atakuwa nalo ni kuongoza timu hiyo ya wachezaji wa kiume wasiozidi umri wa miaka 20 katika Kombe la Afrika almaarufu Barthes Trophy. Kombe hilo lilifaa kuandaliwa jijini Nairobi mwezi Aprili 19-26, lakini likaahirishwa hadi mwaka 2021 kutokana na janga la virusi vya corona ambalo limeua zaidi ya watu 700 nchini Kenya.
Katika dimba hilo, Chipu itakabiliana na Madagascar, Tunisia na Zambia, huku mshindi akijikatia tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia. Chipu iliduwaza miamba Namibia 21-18 katika fainali yam waka 2019 na kushiriki mashindano ya dunia nchini Brazil.