Chipu tayari kuelekea Brazil kwa Raga ya Dunia licha ya changamoto ya kifedha
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya Kenya ya raga ya wanaume ya wachezaji 15 kila upande wasiozidi umri wa wa miaka 20 almaarufu Chipu inatarajiwa kuelekea nchini Brazil mnamo Alhamisi usiku kushiriki Raga ya Dunia ya daraja ya pili (JWRT).
Taarifa kutoka Shirikisho la Raga nchini Kenya (KRU) zinasema kuwa mabingwa hao wa Afrika watatumia ndege ya aina ya Emirates.
Licha ya kuahidiwa usaidizi kutoka kwa serikali ilipofuzu kurejea katika jukwaa hilo la dunia baada ya kuchapa miamba Namibia 21-18 jijini Nairobi mnamo Aprili 7, Chipu imekuwa ikitatizika kuchangisha zaidi ya Sh15 milioni inazohitaji.
Mwenyekiti wa KRU Oduor Gangla alisema Juni 26 kuwa Chipu ina ukosefu wa Sh13 milioni katika bajeti yake ya kuenda Brazil kwa mashindano hayo ya mataifa manane. Alifichua kuwa KRU itaandaa harambee kuchangisha fedha hizo.
Ripoti zinasema kuwa Sh1.2 milioni taslim pekee ndizo zilichangishwa katika harambee hiyo iliyofanyika katika shule ya Peponi mtaani Kabete ambayo iliipa Chipu uwanja, bwawa la kuogelea, nyumba ya kufanyia mikutano na jimu bila malipo.
Matatizo ya kifedha
Kumekuwa na wasiwasi kuwa wenyeji wa makala ya mwaka 2009 Chipu huenda wakajiondoa katika mashindano haya ya kila mwaka kutokana na matatizo haya ya kifedha.
Hata hivyo, afisa mmoja katika shirikisho hilo ameambia Taifa Leo kuwa KRU itafahamu Julai 4 kiasi rasmi cha fedha kilichokusanywa kwa sababu kuna watu ama kampuni zilizotoa ahadi.
Chipu, ambayo inanolewa na kocha wa timu ya watu wazima (Simbas) Paul Odera, itaanza kampeni yake dhidi ya mabingwa wa mwaka 2008 Uruguay (Julai 9), washiriki wapya kabisa Brazil (Julai 14) na washindi wa mwaka 2014 na 2017 Japan (Julai 17) katika mechi za Kundi A mjini Sao Paulo.
Kundi B linajumuisha washindi wa nishani ya fedha mwaka 2014 Tonga (2014), Ureno (2017) na Canada (2013 na 2015) na Hong Kong, ambayo inashiriki makala ya sita mfululizo.
Timu zitakazokamilisha katika nafasi ya kwanza, pili, tatu na nne kutoka Kundi A zitakutana na zile zitakazotamatisha Kundi B katika nafasi ya kwanza, pili, tatu na nne mtawalia kuorodhesha nambari moja hadi nane.
Kenya, ambayo haikuwa imewahi kuwa bingwa wa Afrika licha ya kufika fainali mwaka 2013, 2014, 2016, 2017 na 2018 kabla ya kushinda mwezi Aprili, inalenga kumaliza ndani ya mduara wa nne-bora.
“Tunalenga kumaliza mechi za kundi letu katika nafasi ya pili. Haitakuwa kazi rahisi, lakini tungependa kuhakikishia Wakenya kuwa hatutaaibisha Bara Afrika,” Odera alisema akitaja kikosi chake cha wachezaji 23 watakaosafiri.
Kikosi cha Kenya:
Ian Njenga (Nondies), Bonface Ochieng (Nahodha/Kenya Harlequin), Rotuk Rahedi (Millfield College), Emmanuel Silungi (Homeboyz), Hibrahim Ayoo (Menengai Oilers), James Mcgreevy (Kenya Harlequin), Brian Amaitsa (Nondies), Sheldon Kahi (Blak Blad), Samuel Asati (Nahodha msaidizi/KCB), Dominic Coulson (Nahodha msaidizi/hana klabu), Timothy Okwemba (MMUST), Owain Ashley (Merchiston Castle), John Okoth (Nakuru) Geoffrey Okwach (KCB), Jeff Mutuku (Kenya Harlequin), Wilfred Waswa (Northern Suburbs), Collins Obure (Blak Blad), Ian Masheti (Impala Saracens), Frank Aduda (Impala Saracens), George Kiryazi (Merchiston Castle), Samuel Were (Laiser Hill), Barry Robinson (Kabras Sugar), Douglas Kahuri (Kenya Harlequin), Michele Brighetti (Sedburgh School), Andrew Matoka (Strathmore University), Andrew Simiyu (Afrika Kusini).