Michezo

Chipukizi Haaland wa Dortmund aweka rekodi mpya ya ufungaji katika UEFA

November 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Erling Haaland ambaye ni raia wa Norway, alizidi kuwika kwenye kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya kufunga mabao mawili na kusaidia Borussia Dortmund ya Ujerumani kuwapiga Club Bruges ya Ubelgiji 3-0 mnamo Novemba 4, 2020.

Haaland, 20, alifunga mabao yake mawili katika kipindi cha kwanza baada ya Dortmund kufunguliwa ukurasa wa mabao na Thorgan Hazard ambaye ni kakaye Eden Hazard wa Real Madrid.

Tangu ajiunge na Dortmund mnamo Januari 2020, Haaland amefunga jumla ya mabao 26 kutokana na mechi 28 ambazo amewasakatia miamba hao wa soka ya Ujerumani katika mapambano yote.

Fowadi huyo amepachika wavuni mabao 14 ya UEFA kutokana na michuano 11, idadi hiyo ya mechi ikiwa ndogo zaidi kuwahi kushuhudia mchezaji akijivunia mabao mengi ambayo Haaland amejizolea katika soka ya bara Ulaya.

Rekodi ya awali ya mabao 14 kwenye soka ya UEFA ilifikiwa na Harry Kane wa Tottenham Hotspur baada ya mechi 17 za kipute hicho.

Haaland ambaye anawaniwa pakubwa na Real Madrid, kwa sasa amefunga dhidi ya wapinzani wote saba ambao Dortmund wamekutana nao kwenye kivumbi cha UEFA hadi kufikia sasa.

Hata hivyo, alikosa fursa nyingi za kufunga mabao matatu katika mechi moja baada ya kupata ufanisi huo msimu jana alipofungia waajiri wake wa zamani RB Salzburg ya Austria magoli matatu kwenye mchuano uliowakutanisha na Genk kwenye hatua ya makundi.

Dortmund kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi F kwa alama sita, moja zaidi kuliko Lazio ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).