Chipukizi wa Chapa Dimba na Safaricom wajifunza mengi ugenini
Na JOHN KIMWERE
WANASOKA chipukizi wa timu za taifa za Chapa Dimba na Safaricom Season Two, kwa wavulana na wasichana wamerejea baada ya kukamilisha ziara ya siku kumi waliokuwa wakishiriki mazoezi ya mchezo huo nchini Uhispania.
”Kusema kweli ilikuwa ziara ya kufana hasa kwa baadhi yetu ambao ndiyo mwanzo tuliopata nafasi kuzuru mataifa ya kigeni duniani. Pia tulipata nafasi nzuri kufunzwa masuala ya soka na makocha tofauti nchini humo,” mmoja wa kikosi cha wasichana Yvonne Ogada alisema na kuongeza kuwa kisha mazoezi hayo yaliwafaa zaidi maana baadaye walifanikiwa kuzilemea timu walizoshiriki nazo mechi za kupimana nguvu.
”Miaka ijayo nalenga kuibuka kati ya wachezaji mahiri na kubahatika kusajiliwa kuchezea mojawapo kati klabu za Uhispania,” nahodha wa timu ya wavulana, Mohammed Abdirahim wa Al-Ahly FC alisema.
Chipukizi hao wakiwa nchini Uhispania walijivunia kushinda mechi kadhaa za kirafiki pia kushiriki mazoezi ya viungo.
Baada ya wavualana wa kikosi hicho ‘Chapa Dimba na Safaricom,’ kupoteza mechi ya kwanza mabao 5-3 dhidi ya Reus Deportiu baadaye walizoa ushindi katika mechi ya pili walipopiga Sant Gabriel mabao 2-1. Mabao hayo yalifumwa kimiani na Benjamin Njenga(Shimanzi) na Lual Mengistu(Euronuts). Wasichana walishindwa kuhimili makali ya wenyeji hao na kubamizwa mabao 2-0. H
ata hivyo wanadada hao awali walikuwa wameandikisha ushindi mkubwa wa mabao 6-0 mbele ya Tecnofutbol Ladies FC. Vile vile wavulana walionekana kuimarika walipolazimisha sare tasa dhidi ya Gimnastic Tarragona maarufu Nastic Tarragona kwenye mechi iliyochezewa mjini Futbol Salou, Uhispania.