Michezo

Chipukizi wa Kenya wanyoa Tanzania katika gozi la ufunguzi dimba la Cecafa

Na CECIL ODONGO October 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RISING Stars Jumapili walianza kampeni zao za kuwania ubingwa wa mashindano ya Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa kuititiga wenyeji Tanzania 2-1 katika uwanja wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Ukanda wa Cecafa unatarajiwa kutoa timu mbili ambazo zitashiriki Kombe la Afrika (Afcon Under 20) na Kenya inapigania kuwa kati ya mataifa hayo.

Kiungo Kelvin Wangaya aliweka Kenya mbele kupitia mpira wa ikabu uliochongwa vizuri dakika ya 23.

Alipiga mpira ambao ulipaa juu ya mabeki wa Tanzania na kujaajaa wavuni huku kipa wa Tanzania, Anthony Mpemba, akibaki kutazama tu.

Dakika mbili baadaye, wenyeji nusura wasawazishe lakini kipa Ibrahim Wanzala alizima shuti kali kutoka Sheikhan Khamis.

Fowadi Kelly Madada alipoteza nafasi ya wazi kuongezea Kenya goli dakika ya 31 baada ya mpira aliopiga kupaa juu ya mtambapanya.

Katika kipindi cha pili, Kenya ilirejea kwa kishindo na kubuni nafasi kadhaa za kuongeza mabao.

Straika Louis Ingavi alipokea mpira kutoka kwa Madada dakika ya 47 lakini aliachilia fataki iliyotoka nje.

Hassan Beja na Andreas Odhiambo watajilaumu wenyewe kwa kupoteza nafasi tele za kucheka na wavu kati ya dakika 50-60.

Odhiambo aliongeza uongozi wa Kenya dakika 65 mara hii akiujaza wavuni mpira wa Beja.

Tanzania nusra wapunguze uongozi wa Kenya dakika ya 74 ila mpira wa ikabu wa Valentino Kusengama ulizimwa na mabeki wa Kenya.

Dakika mbili baadaye, Tanzania walipata bao kupitia mpira wa ikabu wa Rahim Mkinyange.

Mnyakaji raia wa Kenya Wanzala alitazama tu mpira ukigonga chini kisha kujaa wavuni.

Wenyeji waliendelea kusukuma Rising Stars wakilenga kupata bao lakini Kusengam akapiga kichwa iliyotoka nje pembamba dakika ya 85.

Nchi ambayo itakuwa mwenyeji wa Kombe la Afrika Under 20 itafahamika mnamo Oktoba 22 wakati ambapo kutakuwa mkutano wa CAF, Addis Ababa Ethiopia.

Senegal ndio mabingwa watetezi wa kipute hicho ambacho kitashirikisha timu za ukanda wa Zoni ya Kati, Zoni ya Mashariki ya Kati, Kusini, Zoni ya Magharibi A na B, Kaskazini na Magharibi ya Kati.