Chipukizi wasaidia Dortmund kuilaza M'gladbach 3-0 katika Bundesliga
Na MASHIRIKA
CHIPUKIZI Jude Bellingham alichangia bao katika ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na waajiri wake Borussia Dortmund dhidi ya Borussia Monchengladbach katika mchuano wa kwanza wa msimu huu katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).
Bellingham, 17, alijiunga na Dortmund mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuagana rasmi na Birmingham ya Uingereza. Alichangia bao la kwanza la Dortmund lililofumwa wavuni na Giovanni Reyna katika dakika ya 35.
Kiungo mvamizi wa Uingereza, Jadon Sancho anayehemewa pakubwa na Manchester United, alichangia bao la pili la Dortmund lililojazwa kimiani na Erling Braut Haaland mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Awali, Haaland alikuwa amefunga penalti iliyochangiwa na Reyna, 17, japo M’gladbach walilalamikia refa kwa kutowapa penalti baada ya Mats Hummels kumchezea visivyo kiungo Marcus Thuram mwishoni mwa kipindi cha pili.
Reyna alikuwa miongoni mwa chipukizi waliopangwa katika kikosi cha kwanza cha Dortmund kilichowajumuisha pia Haaland, 20, Sancho, 20 na Bellingham.
Ushindi wa Dortmund unatazamiwa kumtia motisha zaidi Bellingham aliyefunga bao muhimu katika mchuano mwingine wa wiki iliyopita iliyokutanisha Dortmund na Duisburg katika German Cup. Mchuano wa Septemba 19 ulihudhuriwa na takriban mashabiki 10,000 uwanjani Signal Iduna Park.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO