Michezo

Chuo cha soka kinachonoa wanafunzi kuwa 'Ronaldo' wa kesho

May 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

NATASA (Nakuru Talents and Sports Association), ni timu ya soka inayowaleta pamoja wanafunzi kutoka shule ya msingi ya Lions inayopatikana katikati ya mji wa Nakuru.

Limbukeni hao kuanzia darasa la tano hadi nane, wamejitolea kuhakikisha mchezo wa soka unawafaa kimaisha kwa njia moja au nyingine

Mwanzilishi wake Phanuel Imbusi aliona haja ya kuasisi kikosi hiki yapata miaka mitano iliyopita ili kuwapa wanafunzi ujuzi wa vitabu na kuwaongezea elimu ya kusakata kabumbu.

Upatikanaji wa vifaa muhimu kama vile sare, glavu, nyavu na mipira umesaidia wanafunzi wengi kupata ari ya kujimwaya uwanjani kucheza.

Aidha walimu wa michezo wamekuwa na nafasi kubwa,kuwaelekeza na kuwarekebisha wachezaji hawa wachanga,wasiokoma kutesa katika nyuga za nyumbani na zile za ugenini.

Kikosi kizima cha NATASA kikifanya mazoezi kabla ya kushiriki mechi uwanjani Lions Kaunti ya Nakuru. Picha/Richard Maosi

Anahimiza taaluma isiwe ni ile tu ya vitabuni bali pia ihusishe stadi nyinginezo ambazo hazijapatiwa wakati wa kutosha ili zitambulike.

Phanuel anasema katika ulimwengu wa taaluma sio kila mtu atakuja kuwa mhandisi au daktari,hivyo basi wazazi wawapatie watoto wao fursa ya kujinadi kupitia talanta zao.

Hata hivyo mkufunzi Idd Nickel anasema ni muhimu kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi kwa ajili ya kizazi cha kesho.

Anaamini kupaji kinachotambuliwakwa wakati,huchukua muda mrefu kutengenezeka hadi kikakua cha haiba ya kupigiwa mfano.

Akiwa na zaidi ya wachezaji 50 wanaotengeneza safu ya timu mbalimbali baina ya akina dada na wavulana,juhudi zake zinaelekea kuzaa matunda.

Mwalimu Idd Nickel akiwafundisha wanafunzi wake mbinu za kucheza soka wakati wa mazoezi. Picha/ Richard Maosi

Ameweka vizuri safu ya ulinzi,kiungo cha kati na washambulizi katika kila kikosi cha kwanza, kujaza wachezaji 11.

Alielezea dimba kuwa nia yake mwaka huu ni kuhakikisha wanafunzi wake wanashiriki katika michuano mingi ya kirafiki ili kujifua kwa ajili ya kupata uzoefu wa kutosha.

Ametengeneza ratiba ya kupatana na Kabarak FC, Turi, St Andrews, Menengai miongoni mwa timu zingine zenye vikosi dhabiti

“Pia ninatumia soka kuwashawishi wazazi wafahamu kuwa mbali na kuburudisha mashabiki soka inalipa kwa mfano Victor Wanyama wa Tottenham Hotspurs alianza kucheza mpira akiwa mdogo kwenye mitaa ya Muthurwa Nairobi,” akasema.

Anaamini kuwa wanafunzi wake wamejaliwa uwezo wa kuja kusakata boli hadi kiwango cha kimataifa, endapo watazamia michezo kama taaluma.

Akitumia picha za video kutoka kwa wachezaji nguli ulimwenguni kama vile Cristiano Ronaldo wa Juventus na Sergio Aguero wa Manchester City, anawahimiza wachezaji wake kuiga stadi hizo.

Nahonda wa timu ya NATASA kutoka kaunti ya Nakuru akionyesha ujuzi wake uwanjani. Picha/ Richard Maosi

Baadae zitawafaa pale wanapoingia uwanjani katika hatua ya kushiriki kwenye patashika yenyewe.

Mwalimu Godfrey Barasa naibu kocha anasema,mtaala wa elimu utilie mkazo umuhimu wa kutambua na kulea vipaji miongoni mwa watoto.

Uwasaidie wanafunzi kujipatia ujuzi wa kufanya kazi kwa mujibu wa uwezo wao, ili siku za baadae waje kuwa watu wa kutengeneza nafasi nyingi za ajira.

Wasaidie kufufua sekta ya soka humu nchini ambayo haijatiliwa maanani, na badala yake wawakomboe kutokana na dhana potovu ya kutegemea kisomo tu.

Wajaribu kuratibu wakati wa masomo na ule wa kucheza kwa kuwapatia wanafunzi wakati wa kutosha kufanya mazoezi na kupambana na timu hasimu zilizokubuhu.