Michezo

City Queens wapania kuwa wakali wa soka ya mabinti

June 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

JAPO ni chini ya mwaka mmoja tangu ianzishwe, timu ya City Queens inalenga kujituma kiume kuhakikisha inapiga hatua kwenye kampeni za soka ya wanawake hapa nchini. City Queens ni kati ya vikosi ambavyo kwa mara ya kwanza vinashiriki mechi za kufukuzia ubingwa wa Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu.

Kocha aliye mwanzilishi wake, Derricque Charltone Desh anadokeza kuwa taifa hili limefurika chipukizi wengi tu, wavulana na wasichana ambao hawana timu za kuchezea jambo lililomsukuma kujiunga na vikosi vingine kwenye mkakati wa kupalilia talanta za wasichana wanaoibukia katika Kaunti ya Nairobi.

”Ingawa ndiyo mwanzo tunaanza ligi ya chini tunalenga kufanya kweli na kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki ngarambe ya Ligi Kuu (KWPL) nchini ndani ya misimu mitatu ijayo,” alisema na kuongeza kuwa wanafahamu bayana siyo jambo rahisi lakini lazima wajitahidi kwa udi na uvumba.

Aidha ofisa huyo alisema hata wachezaji waliokamaa ambao hushiriki soka ya viwango vya juu nchini walianzia ligi za mashinani. Kwenye kampeni za kipute hicho msimu huu, City Queens imekamata nafasi ya saba kwa kuvuna alama tatu baada ya kucheza mechi sita inakojivunia ushindi wa mchezo mmoja.

Akitetea kikosi chake alisema wachana nyavu hao hawakuwa wamezoea kushiriki mechi za ushindani mkali. Katika mpango mzima anasema wanalenga kuibuka malkia wa ngarambe hiyo msimu huu.

Kocha huyo anashukuru uongozi wa Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF) Tawi la Nairobi Magharibi kwa kuendesha michezo hiyo vizuri.

Anadokeza kampeni za kipute hicho nazo pia zinashuhudia msisimko mkali hali inayodhihirisha wazi kwamba mchezo huo unazidi kuimarika baada ya maofisa wapya kutwaa uongozi huo.

City Queens inajumuisha wachezaji kama: Walinda lango:Nancy Nyambura, Mitchell Diana Akinyi na Grace Wachera.

Beki: Clavis Engesa (naibu wa nahodha), Lucy Afandi, Silvian Nzindoli, Aisha Mohammed, Prudence Kaveza, Margaret Mbithe na Belinda Imbindiku.

Safu ya kiungo: Valary Atieno, Purity Indeche, Gentrine Lwosi, Joy Tsisika, Maryanne Chepkemoi, Joyce Nyambura, Terry Nyambura, Pauline Mwende, Susan Kagendo, Mercy Amagove, Jane Njeri, Mercy Musimbi na Maureen Adhiambo.

Washambulizi: Shildah Khaika, Jackline Muthoni, Beatrice Mwangi, Anita Redempter, Mercy Njeri, Laura Mugasia na Nancy Amagove (nahodha).

Benchi la kiufundi ni Charltone Desh na Said Fakii mama (kocha na naibu wake), Ann Wanjiku (meneja) na Maureen Adhiambo (daktari wa timu).

Mkufunzi huyo anatoa mwito kwa wahisani wajitokeze kushirikiana nao kusukuma gurudumu la kikosi hicho kwenye jitihada za kukuza talanta za wanasoka chipukizi. Anashauri wachezaji wanaokuja kwamba wanastahili kujituma kushiriki ili kuimarisha mchezo wao.