City Stars, Bidco United zatwaa uongozi wa NSL
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Nairobi City Stars ilichupa juu ya jedwali ya kinyang’anyiro cha Supa Ligi ya Taifa (NSL) baada ya kudhalilisha Northern Wanderers kwa magoli 6-0 kwenye patashika iliyochezewa Hope Center Kawangware, Nairobi.
Nayo Bidco United na FC Talanta zilibeba ushindi wa goli 1-0 na magoli 3-0 mbele ya Modern Coast Rangers na Maafande wa Kenya Police mtawalia huku Nairobi Stima ikilazimishwa kutoka sare tasa na Mt Kenya United.
Washiriki wapya Northern Wanderers inaendelea kufanya vibaya ambapo ilidondosha mchezo wa sita mfululizo kwenye kampeni za kipute hicho.
City Stars ilianza mechi hiyo kwa kasi na kufungua ukurasa wa mabao kupitia Ebrimah Sanneh dakika ya saba. Wafungali wengine walikuwa David Gateri magoli mawili nao Oliver Maloba, Kevin Okumu na Jimmy Bagaya kila mmoja alicheka na wavu mara moja.
Bidco United ilipata ushindi huo licha ya kusalia wachezaji kumi baada ya mwamuzi wa katikati kutuma Francis Oduor benchi.
Nazo St Josephs Youth na maafande wa APs Bomet kati ya timu tano zinazong’ang’a kufa na kupona kutafuta angalau ushindi wa kwanza zilikubali kulala kwa mabao 3-2 na 2-0 mbele ya Vihiga United na Migori Youth mtawalia. Nayo Ushuru inayotiwa makali na kocha,
James ‘Odijo’ Omondi ambayo imetoka nguvu sawa mara tatu ilijikakamua kiume na kubamiza Fortune Sacco bao 1-0 na kurukia nafasi ya sita bora kwa kuandikisha pointi 12.
City Stars kati ya timu tano zinazojivunia kutokuonja kichapo kwenye mechi za msimu huu imetua kileleni kwa msimamo wa kipute hicho kwa alama 16, moja mbele ya Bidco United.