Michezo

City Stars yazidi kutetemesha kipute

March 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Nairobi City Stars iliendelea kutetemesha wapinzani wao kwenye kampeni za kufukuzia taji la Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL) baada ya kuchoma Nairobi Stima bao 1-0 kwenye mechi iliyopigiwa Uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

City Stars maarufu Simba wa Nairobi ilionyesha mechi safi na kuhakikisha inabeba pointi tatu muhimu ili kuendelea kujiongezea matumaini ya kutwaa ubingwa wa taji hilo na kufuzu kushiriki Ligi Kuu ya KPL msimu ujao. City Stars ilipata bao hilo la pekee kupitia juhudi zake, Ebrima Sanneh.

”Mechi hiyo haikuwa rahisi lakini wachezaji wetu walifanya kazi njema ambapo walijitahidi kwa udi na uvumba na kufanikiwa kushinda wapinzani wetu,” alisema meneja wa City Stars, Neville Pudo.

Kwenye matokeo ya mechi nyingine kuwania taji hilo, Administration Police (AP) iliona giza ugenini iliponyukwa mabao 3-1 na wenyeji wao Coast Stima katika patashika iliyopigiwa Uwanjani Mbaraki Sports, mjini Mombasa.

Sajili mpya aliyejiunga na Coast Stima kwa mkopo kutoka Gor Mahia FC, Erick Ombija alitiingia timu hiyo mabao mawili kunako dakika ya 10 na 81.

Bao la tatu lilitupiwa kambani na Rodgers Okumu dakika ya 78. Nacho kikosi cha Mafande wa AP kilipata bao la kufuta machozi dakika ya 85 kupitia juhudi zake Alfred Chole.

City Stars ingali kifua mbele kwa kufikisha alama 61 baada ya kushuka dimbani mara 25.