Michezo

Corona ilikuja wakati nikijivunia fomu ya kutisha, asema Kamworor

May 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia katika mbio za Nusu Marathon, Geoffrey Kamworor amesema kwamba mkurupuko wa virusi vya corona ulitokea wakati ambapo fomu yake ilikuwa bora zaidi katika historia yake ya uanariadha.

Hata hivyo, amesema kwamba atalazimika kuanzia alipofikia kampeni za mbio katika kalenda mbalimbali za riadha zitakaporejelewa msimu huu baada ya janga la corona kudhibitiwa vilivyo.

“Nilikuwa katika fomu ya kutisha gonjwa la Covid-19 lilipobisha. Kukaa nyumbani ni changamoto kubwa na kunahitaji nidhamu ya hali ya juu. Najifanyia mazoezi ya kujiweka sawa ili nisitaabike sana mashindano yatakaporejea. Tarajieni mambo mazuri kutoka kwangu,” akasema Kamworor.

Kamworor alikuwa akizungumza katika mkutano wa mtandaoni ulioandaliwa na Kamati Kuu ya Kitaifa ya Olimpiki kwa nia ya kuwahamasisha wanariadha kuhusu lishe bora wakati huu ambapo ulimwengu mzima wa michezo unazidi kubuni mikakati ya kukabiliana na janga la corona.

Wengine waliowasilisha katika mkutano huo ni mwanamasumbwi wa Olimpiki Elizabeth Andiego na wataalamu wa lishe bora, Erick Kihugwa na Mercy Barwecho.

Mwishoni mwa kikao hicho, Kamworor alisema: “Nashukuru sana vinara wa Nock kwa kuandaa mikutano ya aina hii ambayo itahakikisha kwamba wanariadha wanasalia katika hali shwari kwa kuteua kila wanachokula katika kipindi hiki kigumu cha corona. Natarajia kurudi ulingoni kwa matao ya juu na kutawala mengi ya mapambano ya riadha muhula huu.”

Licha ya shughuli za michezo kukwama katika takriban ulimwengu mzima, Kamworor ameungama kuwa ratiba ya shughuli zake za kila siku haijaathiriwa sana.

“Sijabadilisha kabisa taratibu za lishe yangu. Nimedumisha chakula kile kile ambacho mimi hutumia wakati ninapojiandaa kwa mashindano,” akashikilia Kamworor ambaye ni bingwa wa mbio za New York City Marathon.

Kwa upande wake, Andiego ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kuwakilisha Kenya kwenye Michezo ya Olimpiki mnamo 2012 jijini London, Uingereza, alisema janga la corona limeathiri kwa pakubwa utaratibu wa lishe yake.

“Sijakuwa makini sana na kile ninachokula kwa sababu hatuna mashindano yoyote yanayonukia. Zaidi ya kuathirika kifedha, zipo changamoto tele pia zinazotatiza juhudi za kujipatia chakula mahsusi unachokitamani au kushauriwa na wataalamu wa lishe kukitumia wakati huu wa Covid-19,” akasema.

Barwecho aliwakumbusha wanariadha kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe bora na kula chakula cha kutosha cha kuongeza nguvu mwilini kabla na baada ya kushiriki vipindi kadhaa vya mazoezi.

“Vyakula kama vile viazi vitamu na ndizi ni muhimu sana kwa wanariadha. Mboga na matunda pia ni miongoni mwa vyakula vilivyo na viinilishe bora muhimu na madini yanayohitajiwa zaidi na yeyote anayefanya mazoezi ya mara kwa mara,” akasema Barwechi katika kauli iliyotiliwa mkazo na Kihugwa.