Corona yaileta Spurs balaa ya kifedha
Na CHRIS ADUNGO
TOTTENHAM Hotspur wamechukuwa mkopo wa Sh25 bilioni kutoka Benki ya Uingereza ili kuwawezesha kujiendeshea nyingi za shughuli za klabu na kulipa mishahara ya baadhi ya wanasoka, vibarua, maafisa na wafanyakazi wengine wakati huu wa corona.
Mnamo Mei 29, 2020, Tottenham walifichua kwamba wanatazamia kupoteza kima cha hadi Sh28 bilioni msimu huu iwapo mechi zilizosalia katika kampeni za EPL zitasakatwa bila ya mahudhurio ya mashabiki katika uwanja wao mpya ulio na uwezo wa kubeba hadi watu 62, 303 walioketi.
Hali hiyo iliwachochea kuchukua hatua ya kupunguza mishahara ya vibarua na wafanyakazi wao kabla ya usimamizi kubatilisha maamuzi hayo baadaye kufuatia malalamishi ya wanasoka wa zamani na mashabiki.
Mkopo ambao Tottenham wamepokezwa utarejeshwa pamoja na riba ndogo ya asimilimia tano hasa ikizingatiwa ugumu wa hali ya fedha ambao umeletwa na janga la corona.
“Tumekuwa tukiendesha kikosi hiki kwa kujitegemea kifedha. Asilimia kubwa ya mapato yetu yamekuwa yakitokana na ada za mahudhurio ya mechi miongoni mwa mashabiki,” akasema Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy.
Tottenham ambao wameshiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika misimu minne iliyopita, kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la EPL japo pengo la alama saba zaidi linatamalaki kati yao na Chelsea ambao wanafunga orodha ya nne-bora huku zikisalia mechi tisa zaidi kwa muhula huu kutamatika rasmi.
Mbali na mechi zao za EPL ambazo zilitarajiwa kuwakongamanisha mashabiki wengi uwanjani mwa Tottenham, kikosi hicho kingalijivunia fedha nyingine kwa kutumia uga wao kuwa mwenyeji wa hafla za Guns N’ Roses, Lady Gaga na Capital Summertime ambazo tayari zimeahirishwa. Pigano lililokuwa likutanishe pia mwanamasumbwi Anthony Joshua wa Uingereza na Kubrat Pulev wa Bulgaria ugani Tottenham, limeahirishwa.
Mchuano wa Rugby League pia uliokuwa uwakutanishe New Zealand na Uingereza mnamo Novemba na mechi mbili za National Football League zilizokuwa zifanyike ugani humo mnamo Septemba 2020 pia zimefutiliwa mbali.
Tottenham wanatarajiwa pia kurejesha zaidi ya Sh8 bilioni kwa wapeperushaji wa matangazo yao wakati wa mechi za EPL redioni na runingani.
Levy amekuwa mwenyekiti wa Tottenham kwa takriban miaka 20 iliyopita baada ya kuchukuwa nafasi ya Sir Alan Sugar mnamo Februari 2001.