Corona yailizimu DRC kusitisha ligi
Na CHRIS ADUNGO
JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa nchi ya nane baada ya Kenya, Cameroon, Angola, Burkina Faso, Congo Brazzaville, Mauritius na Niger kutamatisha rasmi kampeni za Ligi Kuu za soka kwa sababu ya janga la corona.
TP Mazembe wametawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya DR Congo baada ya kampeni za soka za taifa hilo msimu huu kutamatishwa kwa sababu ya janga la virusi vya corona.
Katika taarifa yake, Shirikisho la Soka la DR Congo (Fecofa) limesema kwamba lilifikia maamuzi ya kutamatisha rasmi kipute cha msimu huu wa 2019-20 na kutawaza TP Mazembe wafalme mara 18 wa Ligi Kuu baada ya shughuli zote za michezo kusimamishwa nchini humo kutokana na janga la Covid-19.
Hadi kampeni za Ligi Kuu zilipositishwa msimu huu, TP Mazembe walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 53, tano zaidi kuliko AS Vita Club walioambulia nafasi ya pili.
Kwa mujibu wa Fecofa, klabu za OC Bukavu Dawa na AS Nyuki zilizokokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama 14 na 12 mtawalia ziliteremshwa daraja hadi kipute cha Daraja la Kwanza huku JSK na Etoile Jaune zikipandishwa ngazi kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya DR Congo (Super Ligue 1) msimu ujao.
Fecofa pia ilifichua kwamba TP Mazembe na Vita Club kwa sasa watawakilisha DR Congo kwenye kampeni za Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League) msimu ujao huku AS Maniema wakipeperusha bendera ya taifa hilo kwenye kinyang’anyiro cha Kombe la Mashirikisho la Afrika (CAF Confederations Cup).