Michezo

Covid-19 yayumbisha soka mitaani

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

JANGA la Covid-19 limeathiri sekta nyingi ulimwenguni kote ikiwa ni pamoja na biashara, utalii, elimu, michezo, miongoni mwa nyingi nyinginezo.

Hapa nchini Kenya katika sekta ya michezo masaibu yapo tele kuanzia timu za kitaifa hadi klabu mbalimbali za mashinani.

All Stars Githurai na Githurai United, ni miongoni mwa klabu zinazokuza chipukizi wa soka mitaa ya Githurai, Zimmerman, Kahawa West, Kahawa Wendani, Kasarani, na viunga vyake.

Athari za Covid-19 ni bayana katika timu hizo.

Kabla ya janga hili, kila siku kuanzia mwendo wa saa nane adhuhuri, Githurai All Stars na Githurai United zilikuwa zikishiriki mazoezi. Hata hivyo, kufuatia athari za corona, uga wa Githurai, wanakofanyia mazoezi, sasa ni mahame.

Uga huo pia hutumika kufanyia mazoezi ya voliboli, ila sasa umegeuzwa kuwa njia ya mpenyo.

“Tangu Kenya ithibitishe ugonjwa wa Covid-19 na mikusanyiko ya umati wa watu kupigwa marufuku, tumeathirika kwa kiasi kikuu. Hatufanyi mazoezi,” anasema Fredrick Ochieng, mwasisi na mwanzilishi wa timu hizo.

Ni timu iliyokuza vipaji hodari wanaochezea klabu tajika nchini wakiwemo; Kevin Kimani na David Okello (Mathare United), Danson Kago, Kevin Odongo na Samuel Mbugua (Posta Rangers), Francis Kahata (Gor Mahia FC) na Peter Nzuki (Tusker).

Ili kupalilia vipaji chipukizi, Fredrick Ochieng amegawanya mazoezi kwa makundi matano; walio chini ya umri wa miaka 10, 12, 14, 16 na zaidi ya 18.

Timu ya umri zaidi ya miaka 18, imeshiriki michuano ya ligi ya FKF, Super 8 na tonamenti ya Koth Biro.

“Wengi wa vijana wetu wanategemea mapato ya mechi wanazoshiriki kujiendeleza kimaisha na kukidhi mahitaji yao ya kimsingi. Kwa sasa wanahangaika ikizingatiwa kuwa vibarua havipatikani,” Kocha Ochieng anaeleza.

Peter Nzuki, pia mkufunzi wa All Stars Githurai na Githurai United anasema janga la Covid-19 limeathiri makinda wa klabu, wengi ambao wamenusuriwa kutoka kwa visa tofauti vya maovu, kama vile uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya na pombe.

Mkufunzi Peter Nzuki anayewapa ujuzi vijana wa klabu za soka mtaani Githurai. Sekta ya michezo imeathirika kwa kiasi kikuu na janga la Covid–19. Hii ni picha ya kabla ya janga hilo nchini Kenya. Picha/ Sammy Waweru

“Muda wa ziada hasa kwa chipukizi walio shuleni, huuteka kwa mazoezi. Tunawaepusha kushiriki matendo maovu,” Nzuki ameambia Taifa Leo.

Klabu zingine nchini zinapitia yayo hayo.

Nchini Ujerumani ligi kuu ya Bundesliga imerejelewa japo kwa masharti makali.

Kama hilo linawezekana kwingineko ulimwenguni, basi Fredrick Ochieng na Peter Nzuki pamoja na viongozi wengine wa klabu za All Stars Githurai na Githurai United, wana matumaini Kenya itashinda vita dhidi ya virusi vya corona na hali itarejea kama kawaida.