Michezo

Crested Cranes wapata dawa yao Cecafa

July 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Tanzania wameandikisha ushindi wao wa kwanza katika Soka ya Wanawake ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) baada ya kupepeta Uganda 4-1 jijini Kigali, Rwanda, Jumatatu.

Kilimanjaro Queens, ambayo ililimwa 1-0 na Rwanda mnamo Julai 19 na kukabwa 1-1 dhidi ya Kenya katika mechi ya pili Julai 21, ilifufua kampeni ya kutetea taji kupitia mabao ya nahodha Asha Rashid, Donasia Daniel na Asha Hamza Shaban. Daniel alimegea Rashid pasi safi iliyozalisha bao dakika ya 17.

Rashid ‘alirudisha mkono’ kwa kumega pasi murwa iliyokamilishwa na Daniel dakika ya 23. Rashid alipachika bao la tatu dakika ya 45 kabla tu ya mapumziko baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Fatuma Issa.

Tanzania, ambayo ilicharaza Kenya 2-1 katika fainali ya makala yaliyopita nchini Uganda, ilipata bao la nne kupitia kwa Shaban dakika ya 52. Alipokea pasi nzuri kutoka kwa Stumai Abdalla.

Crested Cranes, ambayo ilishangaza Kenya 1-0 katika mechi ya ufunguzi na kulima Ethiopia 2-1 katika mechi ya pili, ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 90.

Cranes inaongoza mashindano haya ya mataifa matano kwa alama sita. Itarukwa na Rwanda ikiwa wenyeji hawa watalemea Ethiopia baadaye Jumatatu. Harambee Starlets ya Kenya haina mechi hadi Julai 25 itakapomenyana na Ethiopia. Starlets ina alama moja. Tukienda mitamboni, Ethiopia haikuwa na alama.