Michezo

Corona ni baraka kwangu, asema Faith Ogallo

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KUAHIRISHWA kwa Michezo ya Olimpiki za 2020 jijini Tokyo, Japan ni baraka tele kwa mshindi wa nishani ya fedha katika mchezo wa taekwondo barani Afrika, Faith Ogallo.

Ogallo alijikatia tiketi ya kunogesha Olimpiki ambazo kwa sasa zimeahirishwa hadi mwakani baada ya kumdengua Florence Eldima kutoka Chad katika michuano ya kufuzu iliyoandaliwa jijini Rabat, Morocco mnamo Februari 2020.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Kibabii anasema kwamba kusogezwa kwa michezo hiyo ambayo kwa sasa itaandaliwa Juni-Julai 2021, kutampa jukwaa mwafaka zaidi la kujiandaa vilivyo.

Ogolla aliyejitosa rasmi katika ulingo wa taekwondo mnamo 2018, sasa anapania kuboresha zaidi maandalizi yake kwa minajili ya Olimpiki na mapambano mengine yajayo kwa kujifanyia utafiti zaidi mtandaoni ili kuimarisha mbinu zake za kuwakabili wapinzani.

“Sina uzoefu mkubwa katika ulingo wa taekwondo ya kimataifa. Naamini kwamba muda uliopo unanitosha kwa sasa kujifua vilivyo kwa minajili ya kibarua kilichopo mbele yangu na kujizolea medali. Nilijitosa katika mchezo huu mnamo 2018 na ninatarajia kujiongezea makali zaidi kabla ya kufunga safari ya kuelekea Japan mwakani,” akasema.

Olimpiki za Tokyo ni mapambano ya tatu ya kimataifa kwa Ogolla kunogesha baada ya kutamba katika Michezo ya Bara la Afrika na kipute cha Fujira Championships kilichoandaliwa Dubai.

Japo anafurahia kwamba kuahirishwa kwa Olimpiki kunampa muda wa kujiandaa vya kutosha, analia kwamba kusimamishwa kwa shughuli zote za spoti za humu nchini kumevuruga pakubwa ratiba yake ya mazoezi kwa kuwa marufuku yanayoharamisha mikusanyiko ya umma yanamnyima fursa ya kushiriki mazoezi ya pamoja na wenzake.

“Kujifanyia mazoezi nyumbani kuna changamoto tele. Nakosa fursa ya kufanya mazoezi ya pamoja na wenzangu ambao walikuwa wakinitilia shime zaidi chuoni,” akasema kwa kusisitiza kuwa maamuzi ya kujitosa katika taekwondo ni zao la kuhimizwa na kocha wa timu ya taifa, Eliachim Otieno.

“Niliwahi kujaribu bahati katika fani mbalimbali zikiwemo mbio za mita 400 kuruka viunzi, voliboli, vikapu na mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji bila mafanikio. Nilifanya haya yote nikisaka fursa ya kuwakilisha taifa katika ulingo wa kimataifa. Ni Otieno ndiye alinishauri kujibwaga katika taekwondo baadaye,” akaongeza Ogolla.