DAGORETTI: Mabingwa wa soka shule za upili Nairobi
Na PATRICK KILAVUKA
NI mabingwa wa soka katika mashindano ya shule za upili Kanda ya Nairobi (Copa Coca Cola) mwaka huu.
Dagoretti ilitawazwa wafalme baada ya kuinyuka Shule ya upili ya Upper Hill 2-0 katika fainali ambayo iliandaliwa Shule ya Upili ya Lenena, Nairobi.
Kulingana na mwalimu Emmanuel Okuna ambaye anasimamia idara ya michezo shuleni humo, mwaka jana ilipoteza kwa kiduchu fainali za mwaka huo kwa kutandikwa 3-1 na Shule ya Upili ya Highway katika robo fainali hali ambayo iliwapelekea kurudi kwenye ubao tena kujisuka kuanzia mwezi Julai, mwaka jana.
Baada kutambua dosari zilizoipelekea kutofanya vyema, wadau wa shule walimtafuata kocha George Ooko wa Bandari kukoleza mbinu ambazo zitainua timu na sasa wamejifunga kibwebwe kuhakikisha timu inatamba wakitazamia kufanya vyema hata katika mashindano ya kitaifa.
“Tuliamua kuijenga timu upya na matunda ya kufuzu katika fainali za kitaifa ni ishara tosha kwamba, mbegu ya timu imeota na kukita mizizi na tunazamia kuwa na timu ambayo itainua jina la shule,” asema Mkufunzi na msimamizi wa idara ya michezo huyo.
Anaongezea kwamba, uhusiano mwema katika kikosi, walimu, mwalimu msimamizi Peter Orero ambaye alikuwa mwalimu msimamizi wa shule tani ya Upper Hill, kinara NRSSSA na naibu rais wa Shirikisho la Michezo la Shule za Afrika Mashariki ( EASSSA) umeifungulia milango timu hii kufika umbali huu.
Kabla kufikia daraja hii ya kinganganyiro hicho, ilikuwa imetawazwa bingwa wa kaunti ndogo ya Dagoretti.
Hata hivyo, ilianza kucheza katika michuano ya makundi ambapo ilitoka bila kupoteza mchuano wowote. Iliichapa Brooyln 6-0, Shule ya upili ya Eylon 2-1 kisha kuigonga Eutycus 7-0 na kufuzu robo fainali. Katika mkumbo huo, iliirambisha sakafu Hidden Talent 5-1 uwanja wa shule ya Upili ya Lenena.
Kwenye nusu fainali ya mashindano ya kaunti ndogo iliirarua Shule ya Upili ya Lenena 2-0 kabla kuendeleza ubabe kwenye fainali na kuitinga Shule ya Mseto ya Dagoretti 4-0 na kupewa shughuli nzima ya kuiwakilishi kaunti hiyo katika patashika la Kanda ya Nairobi (NRSSSA).
Hata hivyo, msuma wa timu uliendelea kuwaka katika kiwango hicho na kupepea pasi na kupoteza mechi yeyote kisha kutangazwa washindi wa mashindano hayo.
Katika michuano ya makundi ya Kanda ambayo iliandaliwa shuleni mwao, iliichabanga Shule ya Wavulana ya Ruai 5-0, kuibwaga Ofafa Jericho 4-1 na kufuzu robo fainali dhidi ya Jamhuri na kuinyeshea mvua ya magoli 6-0.
Halafu ilipiga nusu fainali dhidi Highway na kuidonoa 5-0 na kufuzu kucheza fainali ambazo ziliiwezesha kulibeba taji kwa kuiliza Upper Hill mbili kwa nunge kupitia wafumaji Bonface Mwangami na Oscar Omondi.
Katika kuikuza timu hii kwa miaka na mikaka, Mkufunzi Okuna anasema idara husika ya michezo shuleni kwa ushirikiano wa bega kwa bega na mwalimu msimamizi Orera, imeazimia kuwaalika miamba wa soka nchini kuwarai na kuwahimiza wanasoka hawa chipukuzi jinsi ya kumakinika katika kukuza talanta zao za kandanda.
“Tuna mipango ya kuwakaribisha shuleni sogora wa kabumbu kama nahodha wa Harambee Stars Victor Wanyama na nduguye MacDonald Mariga kuwatia moyo na hamasa wachezaji kuzingatia mwanzo wao mdogo ili wamakinike na wajue kwamba, hata nao walikuwa tu kama wao lakini kupitia bidii ya mchwa, nidhamu na kujitolea wameweza kufikia ufanisi huo kisoka,” asema Okuna na kuongezea kuwa, wanawakuza pia kikademia kwa kuwaweka katika makundi ya kusoma ili wavute kamba yao ya masomo.
Kando na hayo, wanafunzi wanapewa vivutio vya kuwatia motisha kutoka kwa shule, walimu na wahisani katika jamii ambao wanaifuatilia timu wakati inacheza na kuihimiza zaidi.
Kando na timu hii, kuna ya wasiozidi miaka 16 ambayo pia ni moto katika kuchonga vipawa licha ya kwamba ilifika katika fainali za kitengo chao na kunyanyuliwa na watani wao Upper Hill matuta 3-1 baada ya kuagana sare tasa katika muda wa kawaida.
Changamoto? Kizingiti cha timu ni vifaa vya kufanyia mazoezi na gharama za kuiwezesha timu kupiga kambi ya mazoezi kuboresha matokeo zaidi.
Hata hivyo, wito wao ni kwamba, udhamini zaidi unahitajika kuimarisha maandalizi ya timu kuiwezesha kushika dira ya kushiriki katika mashindano ya kitaifa na majaliwa ya Maulana ya Afrika Mashariki kwani wanamini kwamba, safari ya timu imo bandarini na iko tayari kusonga.