• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Dagoretti Mixed na Beijing Raiders mabingwa wa Chapa Dimba Nairobi

Dagoretti Mixed na Beijing Raiders mabingwa wa Chapa Dimba Nairobi

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Dagoretti Mixed na Beijing Raiders zilitawazwa wafalme na malkia katika Mkoa Nairobi, kwenye mechi za Chapa Dimba na Safaricom, Season Three baada ya kuzima wapinzani wao katika fainali.

Wavulana wa Dagoretti Mixed waliibuka mabingwa wa kipute cha msimu huu na kutwaa tikiti kuwakilisha Mkoa wa Nairobi katika fainali za kitaifa. Kwenye fainali hizo zilizopigiwa uwanja wa Shule ya Jamhuri High.

Dagoretti chini ya kocha, Joseph Orao iligonga Hataki Sportiff mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare tasa. Waliofungia Dagoretti walikuwa Hagai Victor, Achoka Peter, Alex Munga na Ghai Mwongela.

Hakati Sportiff ilipata mabao hayo kupitia Jumba Jackson, Juma Julius na Magolo Glen. ”Bila shaka nashukuru wachezaji wangu wote kwa kuzingatia mawaidha yetu kwenye mechi zote nusu fainali na fainali,” alisema kocha wa Dagoretti Mixed na kukiri kuwa wangeteleza katika fainali wangeona giza.

SHUJAA

Kitengo cha wanawake Beijing Raiders iliibuka malkia wa ngarambe ya muhula huu baada ya kuteremsha soka ya kuvutia na kuchoma wapinzani wao bila huruma.

Beijing Raiders ilitawazwa mabingwa wa Mkoa wa Nairobi iliporarua waliokuwa mabingwa watetezi, Acakoro Ladies kwa magoli 6-0 katika fainali ya kusisimua.

Kwenye mechi hiyo, Salome Drailer aliibuka shujaa ambapo alifanya kazi ya nguvu alipoifungia mabao manne kunako dakika ya 40, 59, 72 na 84. Naye mwenzake Facila Adhiambo alicheka na nyavu mara mbili na kuhakikisha wasichana hao wamemaliza shughuli.

SH200,0000

Dagoretti Mixed na Beijing Raiders kila moja ilituzwa kitita cha Sh200,000 kwa kuibuka mabingwa wa kipute hicho katika mkoa wa Nairobi.

Mabingwa hao walibeba tikiti za kushiriki fainali za kitaifa zitakaoandaliwa mjini Mombasa mwezi Juni mwaka huu. Nazo timu zilizomaliza nafasi ya pili kitengo cha wanaume na wanawake kila moja ilipongezwa kwa Sh100,000.

NUSU FAINALI

Kwenye nusu fainali ya wavulana, Dagoretti Mixed na Hakati Sportiff kila moja ilitwaa ufanisi wa mabao 3-0 dhidi ya KSG Ogopa na Brookshine Academy mtawalia.

Nao wasichana wa Acakoro Ladies walijikatia tikiti ya fainali kwa kulaza St Annes Eaglets mabao 5-1. Nayo Beijing Raiders ilikomoa Kibagare Girls mabao 3-0.

”Tulifahamu vizuri kuwa fainali za raundi hii zitashuhudia ushindani mkali wala hatuna budi ila tunashukuru Mola kwa kutuwezesha kuibuka mabingwa na kusonga mbele,” alisema kocha wa Beijing Raiders, Mark Okwiri.

TUZO ZA KIBINAFSI

Salome Drailer wa Beijing Raiders alibahatika kuzoa tuzo mbili kama mfungaji bora wa kike kwa kutupia kambani magoli manne pia kuibuka mchezaji anayeimarika.

Kwa wavulana tuzo ya mchezaji anayeimarika ilimwendea Peter Chibole wa Dagoretti Mixed. Katika hali ya kushangaza wavulana sita waliibuka wafungaji bora baada ya kila mmoja kufungia timu yake bao moja kwenye fainali hizo.

Wao walikuwa Mongai James, Hagai Victor na Felix Okoth wote Dagoretti Mixed. Wenzao wa Hakati Sportiff wakiwa Bandi Lewis, Mutava Lewis na Otieno Juma. Nao Elvis Ochieng (Hakati Sportiff) na Esnas Kisia (Beijing Raiders) walituzwa kama mlinda bora kitengo cha wavulana na wasichana mtawalia.

Dagoretti Mixed na Beijing Raiders zimejiunga na mabingwa wengine kutoka maeneo mengine kufuzu kwa fainali za kitaifa.

Kwa wavulana wamejiunga na wenzao wa Tumaini School (Mkoa wa Mashariki), Berlin FC ya Garissa (Mkoa wa Kaskazini Mashariki, Ulinzi Youth ya Mkoa wa Kati na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.

Wasichana wameungana na Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki), Falling Waters kutoka Mkoa wa Kati na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.

You can share this post!

Wakazi walia nzige wametafuna chakula chote

Mt Kenya United yachomwa 7-2 na Nairobi Stima

adminleo