David Luiz na wenzake wasimama na Sarri licha ya vichapo
NA CECIL ODONGO
MLINZI wa timu ya Chelsea David Luiz amesema kwamba wachezaji wa Chelsea wana imani na utendakazi wa kocha wao Mauruzio Sarri na akaahidi kwamba watazidi kuzikumbatia mbinu zake za ukufunzi.
Hii ni baada ya kocha huyo kulaumu wachezaji wake kuwa wagumu wa kutiwa motisha baada ya kichapo cha 2-0 mikononi mwa mabingwa wa zamani Arsenal Jumamosi Januari 19 katika uwanja wa Emirates jijini London.
Hata hivyo Luiz ameunga mkono kauli ya kocha huyo na kusema kwamba hakuna mchezaji hata moja kikosini aliyefurahishwa na kichapo hicho.
“Meneja hakufurahikia kushindwa kwetu na hakuna aliyefurahi baada ya mechi hiyo. Na hayo ni mambo ya kawaida, kuna kushindwa na kupoteza katika soka” akasema Luiz.
Ingawa hivyo, mwanadimba huyo raia wa Brazil alisema kwamba Chelsea imeimarika sana tangu mwanzo wa msimu wa 2018/19 na wanalenga kufanya marekebisho katika idara chache zilizoonyesha kuvuja ili kutoa ushindani mkali katika kampeni ya kuwania ubingwa wa ligi.
“Ilikuwa vigumu kwa yeyote kuamini kwamba tungeweza kumiliki mpira msimu ukianza lakini tumeonyesha kwamba tunaweza. Sarri amefanya kazi ya kuridhisha na tutazidi kumuunga mkono,” akaongeza Luiz.
Kichapo hicho sasa kimezidisha ushindani katika uwaniaji wa timu zitakazomaliza ndani ya mduara wan nne bora katika ligi. Chelsea sasa wapo mbele ya Arsenal na Manchester United kwa alama nne pekee.