• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
De Bruyne, Lewandowski na Neuer kuwania taji la Uefa la Mwanasoka Bora wa Mwaka

De Bruyne, Lewandowski na Neuer kuwania taji la Uefa la Mwanasoka Bora wa Mwaka

Na MASHIRIKA

WANASOKA Kevin De Bruyne na Lucy Bronze Manchester City wameteuliwa kuwania tuzo za Uefa za Mwanasoka Bora wa Mwaka 2019-20 kwa upande wa wanaume na wanawake mtawalia.

Mkufunzi Jurgen Klopp wa Liverpool pia yuko kwenye orodha ya watakaowania taji la Kocha Bora wa Mwaka baada ya kuongoza kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miongo mitatu mnamo 2019-20.

Klopp atapania kubwaga kocha Hansi Flick wa Bayern na Julian Nagelsmann wa kikosi cha RB Leipzig nchini Ujerumani.

Bronze ambaye ni beki wa kulia raia wa Uingereza, alijiunga upya na Man-City kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa mwezi huu Septemba.

Ndiye aliyetawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka katika tuzo za Uefa mnamo 2018-19.

De Bruyne, 29, alitawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka 2019-20 katika tuzo zilizotolewa na Chama cha Wanasoka (PFA) mwanzoni mwa Septemba 2020.

Nyota huyo raia wa Ubelgiji sasa atatoana jasho na Robert Lewandowski wa Poland na Bayern Munich na kipa wa Ujerumani, Manuel Neuer ambaye kwa sasa anawadakia Bayern ambao walitawazwa wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu uliopita.

Tuzo za Uefa kwa wanasoka bora wa mwaka wa 2019-20 zitatolewa mnamo Oktoba 1, 2020, wakati wa droo ya mechi za makundi za Klabu Bingwa Ulaya na Europa League kwa minajili ya msimu mpya wa 2020-21.

Bronze, 28, alitia kapuni taji la tatu mfululizo la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) akivalia jezi za Lyon msimu uliopita kabla ya kurejea Man-City. Atakabiliana na ushindani mkali kutoka kwa Pernille Harder wa Chelsea na Wendie Renard wa Lyon.

Kwa upande wake, De Bruyne alifunga jumla ya mabao 13 ya EPL katika msimu wa 2019-20 na kuchangia mengine 20. Ni ufanisi uliomfanya kufikia ufanisi wa aliyekuwa nahodha na fowadi matata wa Arsenal, Thierry Henry.

Lewandowski alifungia Bayern mabao 55 kutokana na mechi 47 na akawasaidia miamba hao wa soka ya Ujerumani kunyanyua mataji ya Bundesliga, German Cup na UEFA.

Kipa Neuer hakufungwa katika mechi sita za UEFA.

Kwa mara ya kwanza, kitengo cha Kocha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake kitakuwepo katika tuzo za Uefa. Lluis Cortes wa Barcelona atalenga kuwapiga kumbo Stephan Lerch wa VfL Wolfsburg na Jean-Luc Vasseur wa Lyon.

You can share this post!

Frank de Boer apokezwa mikoba ya timu ya taifa ya Uholanzi

JLAC yamuidhinisha Ann Nderitu awe msajili wa vyama vya...