• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
De Gea awania unahodha sasa akilenga kuinua timu

De Gea awania unahodha sasa akilenga kuinua timu

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

BAADA ya kukubali kusaini mkataba mpya kuendelea kuichezea Manchester United, mlinda lango David de Gea sasa anataka apewe unahodha wa klabu hiyo kuanzia msimu ujao, baada ya Antonio Valencia kuondoka.

Ripoti kutoka Old Trafford zimesema kuwa kipa huyo mwenye umri wa miaka 28 amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka sita ambao utamfanya kulipwa kati ya Sh52.5 milioni na Sh56.2 milioni kwa wiki.

Mashabiki wa Manchester wameeleza furaha yao baada ya kusikia kwamba kipa huyo atakuwa klabuni hadi mwaka 2025.

Klabu za PSG na Juventus zimekuwa zikiripotiwa kuwania saini ya raia huyo wa Uhispania ambaye alijiunga na Manchester United mwaka 2011 kutoka Atletico Madrid ya Uhispania.

Mshahara wa sasa wa De Gea ni Sh30 milioni kwa wiki, na sasa nyongeza hiyo itamfanya kuwa kipa anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani.

Mazungmzo kati ya maajenti wa kipa huyo na wawakilishi wa Manchester United yamechukua zaidi ya mwaka mmoja huku ikidaiwa kuwa mlinda lango huyo alihitaji kulipwa mshahara mkubwa zaidi kama ilivyokuwa winga Alexis Sanchez aliyetokea Arsenal.

Hata hivyo, kipa huyo hakuonyesha kiwango kizuri baada ya kuruhusu mabao mengi katika historia ya klabu hiyo kwenye ligi kuu ya EPL.

Itakumbukwa kwamba katika miaka mitano ya hivi karibuni, kipa huyo alitwaa tuzo ya Kipa Bora wa Manchester United.

Mtandao wathibitisha

Mtandao wa Manchester United ulithibitisha habari hizo kupitia kwa ujumbe uliosema: “Makubaliano yamefikia pazuri, sasa De Gea atasaini mkataba wa muda mrefu wa kuendelea kuwepo hapa, uwezo na ubora wake kila mmoja anaufahamu.”

“Hatuwezi kuruhusu wachezaji wetu bora kuondoka kikosini, De Gea ni miongoni mwa wachezaji wetu tegemeo, pia ni mchezaji muhimu zaidi hapa,” alisema kocha wa klabu hiyo, Ole Gunnar Solskjaer.

Katika mechi ya majuzi akiwa langoni, Manchester waliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Inter Milan ya Italia, mfungaji wa bao hilo akiwa Mason Greenwood.

“Nimewahi kupewa majukumu ya kuwa nahodha kwenye mechi kadhaa na sioni ugumu wa kutekeleza wajibu huo tena. Niko tayari kabisa kuifanya kazi hiyo na kulinda vyema beji ya klabu,” aliongeza.

“Kwa hakika, nitafurahi zaidi iwapo nitapewa jukumu hilo muhimu. Nina ujuzi wa kutosha baada ya kuisaidia klabu hii kutwaa ubingwa wa EPL, FA Cup, EFL Cup na Europa League,” alisema.

“Niko tayari kuonyesha uwezo wangu uwanjani, mbali na kusaidia wachezaji chipukizi kuelewa maana ya Manchester United. Ni wakati wa kujitahidi zaidi na kushindani mataji,” aliongeza.

You can share this post!

Zidane akana dai la kumdharau Bale

Migne ataka Stars kuwa macho dhidi ya Tanzania CHAN

adminleo