Dereva Jim Heather-Hayes atawazwa mwanamichezo bora mbio za magari baada ya kufariki
NA GEOFFREY ANENE
MWENDAZAKE Jim Heather-Hayes ametawazwa mwanamichezo bora wa mwaka 2023 wa Shirikisho la Mbio za Magari nchini Kenya (KMSF).
Heather-Hayes alikuwa dereva maarufu katika mbio za magari enzi zake.
Alifariki mwaka 2022 na alikuwa mmoja wa madereva waliovuma katika mashindano ya magari na ametambuliwa kwa mchango wake wa muda mrefu katika mchezo huo.
Heather-Hayes alichangia pakubwa katika kulea mabingwa wa siku zijazo.
Matokeo yake mazuri kabisa katika mbio za magari za Safari Rally yalipatikana mwaka 1990 alipomaliza nambari sita kwa jumla.
Heather-Hayes alishiriki Safari Rally kwa mara ya kwanza ikiwa duru ya Mbio za Magari Duniani (WRC) mwaka 1984 ikidhaminiwa na Marlboro.
Mwenyekiti wa KMSF, Maina Muturi alivulia kofia Heather-Hayes akisema kutuzwa kwake ni ushahidi tosha wa kujitolea kwake na bidii pamoja na ari yake katika michezo ya magari kwa miaka mingi.
Bw Maina aliongeza kuwa Heather-Hayes alionyesha kujitolea katika mchezo huo na kumfanya mtu aliyestahili tuzo hiyo iliyoanzishwa miaka ya 1960.
Hafla hiyo ya KMSF ya kuwapa zawadi wanamichezo waliong’aa katika michezo ya magari hufanyika kila mwaka.
Waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana, Bw Ababu Namwamba na Katibu, Peter Tum pia walimpa zawadi mfalme wa mbio za magari za Afrika Karan Patel na bingwa wa mbio za magari za Afrika za chipukizi Hamza Anwar.
Miongoni mwa mabingwa wa msimu 2023 waliozawadiwa kwa sababu ya kazi nzuri ni ndugu Jasmeet Chana na Ravi Chana walioshinda Mbio za Magari za Kitaifa nchini Kenya (KNRC) na pia kitengo cha B13.
Jasmeet ni mmoja wa madereva wachache ambao wameshinda karibu kila kitengo katika mbio za magari nchini, ikiwemo Kundi N, Madaraja ya Kwanza na Tatu na 2WD katika miaka yake ya kwanza katika fani hii.
Tim Jessop, ambaye alielekeza dereva Carl Tundo kunyakua mataji matano ya duru ya Afrika ya Safari Rally, alituzwa mshindi wa jumla wa mbio za kitaifa za Rally Raid.
Ndugu Chantal na Zane Young waliibuka washindi wa kitengo cha vigari cha Rally Raid.
Nyota anayeinuka kwa haraka Neel Gohil alitunukiwa zawadi ya kutwaa ubingwa wa mbio za vigari za kitaifa za Autocross.
Eric Bengi, John Kadivani na Azaad Manji walishinda Autocross katika vitengo vya magari ya 4WD-T, wazi na 2WD-T.
Namwamba, ambaye alikuwa mgeni wa heshima, aliahidi kuimarisha hadhi ya KNRC na fani mbalimbali za magari ili kuhakikisha kuwa Wakenya wanajiandaa vyema kwa duru ya dunia ya Safari Rally.
“Hatuwezi kujisifu kuwa na mashindano magumu na yanayofahamika kote duniani ya WRC halafu ligi ya hapa nyumbani haina nguvu. Ningependa kuomba wadhamini na wahisani kushirikiana nasi ili kuhakikisha tunapata ubora tuliokuwa nao katika mbio za magari miaka ya nyuma,” alisema Bw Namwamba.
Hafla ya kutuza wanamichezo wa mbio za magari iliandaliwa katika hoteli ya kifahari ya Carnivore jijini Nairobi na kuhudhuriwa na wageni kutoka nje ya Kenya, wakiwemo marais wa mbio za magari Christian Gakwaya (Rwanda) na Dipu Ruparelia (Uganda).
WASHINDI WA TUZO ZA KMSF MWAKA 2023:
Rally Raid
Bingwa wa Rally Raid – Tim Jessop
Dereva bora wa Rally Raid – Alasdair Keith
Mwelekezi bora wa Rally Raid – Charles Mousley
Dereva bora wa kitengo cha Prototype – Mark Glen
Mwelekezi bora wa kitengo cha Prototype – Douglas Rundgren
Dereva bora wa kitengo cha Modified – Alasdair Keith
Mwelekezi bora wa kitengo cha Modified – Charles Mousley
Dereva bora wa vigari vya Buggy – Zane Young
Mwelekzi bora wa vigari vya – Chantal Young
Tarmac
Kitengo cha 4WD – Leroy Mwamba
Kitengo cha 2WD – Moses Mwendwa
Karting
Kitengo cha Bambino – Wilf Mulyanga
Kitengo cha kadeti – Bixente Rio Wyles
Kitengo cha Rotax Junior Max – Krrish Vadgama
4 x 4
Dereva mwanafunzi – Gabriel Lauvaux/Mwelekezi mwanafunzi – Olivier Lauvaux
Dereva wasta – Ben Waiyaki/mwelekezi wasta – Prabjot Saimbi
Dereva stadi – Gurashish Singh/ mwelekezi stadi – Kunal Patel
Dereva stadi kabisa – Oliver Lauvaux/mwelekezi stadi kabisa – John Herbert
Autocross
Kitengo cha Kwanza – 2wd Non-Turbo Buggy: Neel Gohil
Kitengo cha Pili – 2wd Non-Turbo Car: Neel Gohil
Kitengo cha Tatu – 2wd Turbo Buggy: Azaad Manji
Kitengo cha Nne – 4wd Non-Turbo: Jose Sardinha
Kitengo cha Tano – 4wd Turbo: Eric Bengi
Kitengo cha Sita – Open: John Kadivane
Kitengo cha Nane – Bambino: Eann Bengi
Kitengo cha Tisa – Junior 2wd Non-Turbo: Karamveer Singh Roopra
Kitengo cha 10 – Peewee: Allan Bengi
Washindi wa Mbio za Magari za Afrika (ARC)
Dereva: Karan Patel/Mwelekezi: Tauseef Khan
Washindi wa KNRC
Classic: Dereva Ian Duncan/mwelekezi: Jaspal Matharu
2wd: Dereva Daren Miranda/mwelekezi: Linet Ayuko
SPV: Dereva Jose Sardinha/mwelekezi Shameer Yusuf
S: Dereva Kush Patel/mwelekezi: Mudasar Chaudry
Rally Raid: Dereva Chinu Matharu/mwelekezi: Raju Chaggar
B13: Dereva Jasmeet Chana/mwelekezi: Ravi Chana
N: Dereva Nikhil Sachania/mwelekezi: Deep Patel
Rally 3: Dereva McRae Kimathi/mwelekezi: Mwangi Kioni
Rally 2: Dereva Samman Vohra/mwelekezi: Alfir Khan
Mabingwa wa jumla wa KNRC: Dereva Jasmeet Chana/mwelekezi: Ravi Chana