Michezo

DIMBA PWANI: Malengo yetu hayana pupa, Mwatate All Stars wasisitiza

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

‘MWENDA pole hajikwai’ ni msemo ambao meneja wa timu ya Mwatate All Stars FC, Fredrick Msanii, anautumia kujikumbusha wanavyopiga hatua kwa utaratibu tangu klabu hiyo kuanzishwa mwaka 2007.

Meneja huyo asema kuwa hawana haraka ya kupanda ngazi kutimiza maono yao ya kuwa mojawapo ya timu za Mkoa wa Pwani kushiriki kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

“Tumekuwa na subra tukifahamu kwamba ili kufikia malengo yetu hatuhitaji kwenda kwa kasi. Tukifanya hivyo, tutaanguka na kurudi tulikotoka katika ligi ya mashinani. Ndiposa tuliamua mapema kwenda aste aste, na tayari tumeanza kuona dalili za mafanikio,” akasema Msanii kwenye mahojiano na Dimba.

Mwatate All Stars ilikuwa kwenye Ligi ya Kaunti ya Taita Taveta na imekamilisha mechi zake za Kanda B ikiwa kileleni. Timu hiyo ambayo ilijizolea pointi tisa katika mechi nne za Kanda B sasa inajiandaa kwa mechi za Ligi Ndogo za kufuzu kupanda ngazi hadi Ligi ya FKF Pwani Kusini.

“Tunasubiri ratiba za ligi ndogo ili tuanze kupigania fursa ya kupanda ngazi hadi ligi ya mkoa. Tumepania mara hii lazima tupande: kikosi chetu kiko imara na kinaweza kushiriki ligi hiyo ya mkoa na hata kuibuka washindi,” akasema meneja huyo wa Mwatate All Stars.

Kocha Mkuu Peter Kinuthia aliambia Dimba kuwa wanasubiri kwa hamu kushiriki kwenye ligi hiyo ya chini wakitarajia kushinda taji na pia kufuzu kupanda ngazi hadi Ligi ya Pwani Kusini, ambayo nayo mshindi wake anapanda hadi Ligi ya Taifa Daraja la Pili.

“Tumeanza kujiandaa kwa mechi hizo za ligi ndogo. Tuna matumaini makubwa ya kufanya vizuri na hivyo kufanikisha lengo letu la kupanda daraja hadi ligi ya mkoa msimu unaokuja. Tunachosubiri ni ratiba, maandalizi yetu tayari tumeyakamilisha,” alieleza Kinuthia.

Mkufunzi huyo aliongeza kuwa wamewaandaa wanasoka wenye vipaji ambao kwa wakati huu wanachezea klabu za juu humu nchini na ng’ambo.

“Tuna wachezaji watano tuliowaruhusu kusajiliwa na klabu mbalimbali. Mmoja yuko Ujerumani anakochezea klabu ya ligi ya chini,” alisema Kinuthia.

Wasajiliwa kwingineko

Wanasoka waliosajiliwa kwingineko kutoka Mwatate All Stars FC ni pamoja na Babu Kilinda, Jesse Were, Janusas Mandela (Fortune Sacco FC), Dan Gitonga (Taita Taveta All Stars), Gideon Mwamburi (Mwatate United) na Duncan Mwanjare ambaye anachezea Ujerumani.

Kikosi kilichosalia ni kina Fredrick Mwandoe (Nahodha), John Terry (naibu Nahodha), Osinel Mwakireti, Michael Oloo, Michael Mwarandu, Julius Nyange, Ali Mansour, Steven Rendell na Wilmet Mwakera.

Wengine ni Dennis Maina, Francis Joto, Joseph Sadam, James Joshua, Raphael Akama, Swahib Said, Fredrick Juma, Simon Kilimo, Suleiman Nyange, Ali bakari, Kelvin Mashamba, Zuberi Mulasi, Gabriel Mwakise, Ben Mbole na Muli Ruphuse.

Timu ya Mwatate All Stars iliundwa 2007 waanzilishi wake wakiwa Fredrick Msanii na Suleiman Nyange. Nia yao ni kuwafanya vijana washiriki michezoni, wainue vipaji vyao na wajiepushe na matumizi ya dawa za kulevya na maovu mengine.

Kwa misimu miwili mfululizo, timu hiyo imefanikiwa kuibuka washindi wa kombe la Carbon Cup. Iko na vikosi vya vijana wenye umri wa chini ya miaka 13, 17 na 19.

Mbali na kuwa na timu za soka ya wanaume, klabu hiyo ya soka pia ina vikosi vya wanawake.

“Tunaamini timu zetu zote zitafanikiwa kutimiza malengo yetu ya kukuza ta wachezaji wenye vipaji,” alisema Msanii.